File:
12 May 2012
HATIMAYE Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, imekiri kuwepo kwa
ufisadi mkubwa wa kulipa mishahara hewa, ikiwemo ya watumishi wake waliostaafu
na wale waliofariki dunia.
Kutokana na ukweli huo, halmashauri hiyo tayari imemsimamisha kazi mtumishi
wake aliyekuwa anahusika na ulipaji wa mishahara watumishi, Anjelina Kamugisha,
ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo nzito za ufisadi.
Imeelezwa kwamba, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ya Magu ambao kwa
sasa ni marehemu pamoja na watumishi waliostaafu kazi, kwa muda mwingi wamekuwa
wakiingiziwa malipo ya mishahara yao kwenye benki ya NMB tawi la Magu, kisha
fedha hizo kutolewa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana
na baadhi ya watumishi wa benki hiyo wasio waaminifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ya Magu, Cornel Ngudungi (DED),
aliyathibitisha hayo jana jioni, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya
tuhuma za ubadhilifu huo, katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani,
kilichoketi chini ya mwenyekiti wake, Boniventure Kiswaga mjini humo.
Mheshimiwa mwenyekiti, taarifa za halmashauri kulipa mishahara kwa marehemu
na wastaafu, ni kweli zipo. Nimelazimika kuzifuatilia hadi kwa uongozi wa NMB.
“Mishahara hii ilikuwa ikiingizwa benki ya NMB tawi la hapa Magu. Baada ya
kuingizwa ilikuwa ikitolewa na baadhi ya watumishi wetu kwa kushirikiana na
wale wa benki wasiowaaminifu.
“Kwa hiyo, nimeamua kumsimamisha kazi Anjelina Kamugisha ambaye ndiye
aliyekuwa anasimamia ulipwaji wa mishahara. Tuhuma hizi za mishahara hewa zipo
na tunazifanyia kazi”, alisema Mkurugenzi Ngudungi bila kutaja idadi ya fedha
za mishahara hewa zilizolipwa.
Madiwani wa Halmashauri ya Magu wakifuatilia mjadala mkali wa halmashauri hiyo kulipa mishahara kwa watumishi wa halmashauri hiyo ambao walishafariki dunia na wale waliostaafu kazi |
Inasadikiwa kwamba, halmashauri hiyo imetumia mamilioni ya fedha kulipa
mishahara hewa kwa wastaafu na watumishi wake waliotangulia mbele ya haki, nasi tutaendelea kuchokonoa kiundani zaidi ili kubaini idadi halisi ya fedha hizo
zilizotumika vibaya.
Aidha alieleza kwamba, ili kubaini ukweli wa mambo, yeye alilazimika kuonana
na uongozi wa NMB tawi hilo la Magu, kwa lengo jema la kupata usahihi wa
taarifa hizo, lakini aliombwa aende jijini Mwanza akaonane na Meneja wa NMB
Kanda ya Ziwa.
Alisema, baada ya kuonana na meneja huyo aliyemtaja kwa jina la Chilongola,
alielezwa kwamba, benki hiyo haiwezi kutoa fedha hizo mpaka vyombo vya dola,
ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), na jeshi la
polisi waamue kutolewa kwa fedha hizo na si vinginevyo.
“Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Bwana Chilongola aliniambia hawawezi
kuzungumzia suala hilo hadi wapeleke barua.
“Na tulipopeleka barua alitujibu benki yake haiwezi kutoa fedha hizo mpaka
TAKUKURU au polisi waamuru kutolewa kwa fedha hizo”, alifafanua Mkurugenzi huyo
wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Magu, huku akimuonesha mwenyekiti Kiswaga
majibu ya barua ya NMB.
Alisema, tayari alishamwandikia barua Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya hiyo
ya Magu, akimuomba asaidie kupata taarifa ya ripoti ya ukaguzi wa NMB, na
kwamba amemuagiza Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo aanze mara moja ukaguzi
wa wizi huo, pamoja na kutoa ushirikiano zikiwemo nyaraka zote kwa Mkaguzi.
Awali, kulikuwepo na taarifa za halmashauri hiyo kulipa mishahara hewa,
ikiwemo ya watu waliofariki dunia na wale waliostaafu kazi katika halmashauri
hiyo, lakini ukweli wake ulikuwa haujabainika.
Taarifa hiyo, imekuja kufuatia kikao kilichopita cha baraza la madiwani wa
Magu, ambacho kilitoa maazimio ya kuitaka ofisi ya Mkurugenzi kufuatilia tuhuma
hizo, na kikao cha juzi atoe taarifa ya tuhuma hizo za ubadhilifu wa mali ya
umma.
Licha ya Mkurugenzi Ngudungi kutoa taarifa hiyo ya utekelezaji wa baraza la
madiwani, lakini madiwani wenyewe walichachamaa na kumtaka Mkurugenzi huyo
aeleze kwani ni nani aliyekuwa anaidhinisha mishahara ya watumishi, ikiwemo
mishahara hiyo hewa.
Diwani wa Kata ya Lubugu, Julius Ngongoseke (UDP), alisimama na kumtaka
Mkurugenzi Ngudungi alieleze baraza hilo kama kuna mtu tofauti na Mkurugenzi
anayeidhinisha kulipwa kwa mishahara hiyo.
Kufuatia hali hiyo ya vuta ni kuvute, mwenyekiti wa halmashauri
hiyoanayesifiwa kwa umakini katika kazi zake, alilazimika kuvunja kanuni kisha
kusimama kikaoni na kuwaomba madiwani wasiendelee kulijadili suala hilo, kwani
kufanya hivyo wanaweza kutoa fursa ya mtuhumiwa kulalamika kwamba amejadiliwa
mapema, hivyo liachwe lishughulikiwe kisheria zaidi.
No comments:
Post a Comment