Wednesday, March 20, 2013

Ukweli kuhusu Lwakatare

WAKATI Mkurugenzi wa Usalama na Ulinzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilfred Lwakatare akifikishwa kizimbani kwa makosa ya ugaidi, mjadala kuhusu video inayodaiwa kumwonyesha akipanga njama za kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communication Ltd, Dennis Msacky umeshika kasi na kuacha maswali mengi, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Mjadala huo umeshika kasi hasa ndani ya wanachama wa CHADEMA ambao wanaamini si jambo la kupuuzia kwani lina matokeo makubwa sana kwa siasa, demokrasia, usalama, intelijensia na dhamira ya wanamageuzi kutaka mabadiliko ya watawala.
Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na nani alimrekodi Lwakatare? Swali hili ni muhimu kwa maana ya kwamba kama siyo vyombo vya usalama (undercover) huyu aliyemrekodi ni nani?
Je, mtu huyo alikuwa na mamlaka ya kumrekodi? Je, katika kuingilia mawasiliano ya mtu hajavunja haki za kikatiba? Kama mtu yeyote anaweza kutumia ushahidi wa video aliyerekodi mwenyewe bila kupewa mamlaka na polisi au vyombo vya upelelezi je, inawezekana watu wakamtega rais, waziri mkuu au kiongozi wa umma kwa kipimo hicho hicho na polisi watatoa uzito ule ule?
Je, ushahidi ulitunzwaje tangu uchukuliwe Desemba mwaka jana? Swali na changamoto kubwa ni kwamba video hiyo na nyaraka nyingine hazikuchezewa?
Kama ushahidi umekusanywa na raia tu na akakaa nao kwa miezi mitatu (tangu Desemba hadi Machi) swali linapaswa kuuliza je, mkanda huo umekuwa salama muda huo wote? Nani mwingine aliyeuona na kuupitia?
Kama ambavyo video hiyo inavyoonekana imetolewa kwenye mtandao wa Youtube, swali kabla ya video hiyo kusambazwa, ilikuwa wapi na kwa nani?
Kwa wale wanaojua mambo ya audio/visual technology, siyo kazi kubwa sana kubadilisha kitu chochote ambacho kiko kwenye mfumo wa kidijitali. Kuanzia sauti, picha na hata mazingira yanaweza kubadilishwa vizuri tu kwa kutumia kompyuta.
Pamoja na ushahidi huu, ni jukumu la vyombo vya usalama kuhakikisha vinakusanya ushahidi mwingine ili kuupa nguvu ushahidi walionao.
Hii ndiyo sababu ya vyombo vya usalama kwenda kupekua nyumbani kwa Lwakatare na baadaye katika ofisi za CHADEMA.
Wadadisi wa duru za siasa nchini wanasema kuwa endapo ushahidi wa video hii iliyorekodiwa na kurushwa kwenye mtandao utakubaliwa na mahakama, mlango mpya wa vita dhidi ya ufisadi utakuwa umefunguliwa.
Wananchi mahali popote walipo wataweza kutumia simu na nyenzo zao mbalimbali kuwarekodi wahalifu wa kila njama za rushwa au wakipokea rushwa na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao bila kujulikana, na polisi watatakiwa kufanyia kazi bila kulazimika kujua nani amerekodi au kama katika kurekodi taarifa zimebadilishwa kwa namna fulani.
Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema kuwa ukiiangalia video hiyo, utabaini kuwa kipande kinachoonesha sehemu ya mpango au mkakati wa kufanya hivyo ni kweli na kipande cha pili kinaonesha kwamba video hiyo ni feki na imetengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu kuweza kufanya ionekane njama ikipangwa.
“Katika hilo la kwanza inaonekana ndio msimamo wa polisi, Lwakatare amekamatwa, kusachiwa nyumbani kwake na kulala rumande kuendelea na mahojiano na hatua nyingine.
“Inaonekana polisi wanaamini kuwa video hiyo ni kweli inaonesha njama za aina hiyo na ndiyo maana wamechukua hatua. Na ni kutokana na hili bila ya shaka ndiyo maana wamemfikisa mahakamani,” alisema mhadhiri huyo.
Alisema hata kama video hiyo ni ya kweli na haijachakachuliwa, haitoshi bado kuwa ushahidi wa mpango uovu wowote hasa kama sehemu yake ya mwanzo (ilikoanzia) na mwisho wake (ilikoishia) havipo.
“Kwa kutegemea kipande cha katikati tu bado video hiyo inakosa muktadha wa kueleweka. Ni muhimu kwa polisi kuhakikisha wanapata sehemu ya mwanzo na ya mwisho ya video hiyo ili kuweza kuelewa. Hili wanaweza kupata kutoka kwa huyo aliyenao huo mkanda au aliyechukua video. Wanaweza kumuomba awapatie mkanda mzima na ninaamini mawakili wa Lwakatare nao watadai waone mkanda mzima siyo sehemu tu kama ilivyooneshwa,” alisema.
Kama si kweli
Kama sakata zima la Lwakatare sio la kweli, basi wanachama na mashabiki wa CHADEMA wanapaswa kuendelea na harakati za mabadiliko kwani bila shaka kuelekea 2015 yanaweza kuibuka mambo mengi makubwa.
Kama suala zima la Lwakatare si kweli, polisi bado wana jukumu la kuhakikisha wanamtafuta na kumpata mtu aliyetengeneza mkanda huo na kumtia mbaroni kwani anafanya uchochezi kama wanavyomtuhumu Lwakatare.
Tena mtu huyo anaweza kufanya uchochezi wa hatari zaidi kwa namna yake kwani amejaribu kuwaaminisha wananchi kuwa chama kizima cha kisiasa kinahusika na matukio ya utekaji nyara kama mtu kasoma maelezo ya huyo aliyeiweka kwenye mtandao video hiyo, kwani hakuishia kumtuhumu Lwakatare tu bali CHADEMA kama chama na viongozi wake wakuu.
Hata hivyo, jukumu la kuthibitisha ukweli wa video hiyo kama inaweza kukubaliwa kuwa ni ushahidi liko mikononi mwa polisi.
Haitoshi tu kusema Lwakatare ameonekana akisema hili au lile; ni jukumu la polisi kuonesha kuwa ushahidi huo umepatikana kwa njia halali na ambao haukuharibiwa kwa namna yoyote ile.
Kama sio kweli na mahakama ikashindwa kuwatia hatiani wahusika, basi uongozi wa polisi nao utatakiwa uwajibike kwa kuboronga uchunguzi huu na zaidi ya hapo itabidi ihakikishe kuwa wahusika waliotengeneza video hiyo (kama imechakachuliwa) nao wanakutana na mkono wa sheria vile vile.
Na hata kama itaonekana ni kweli Lwakatare alisema anayodaiwa kusema, ni jukumu la polisi kuonesha kuwa alikuwa amevunja sheria.
Kama ni kweli
Kama ni kweli Lwakatare amehusika na mkanda ni wake, basi Jeshi la Polisi halina jinsi isipokuwa kufuata mwanzo wa hilo sakata hadi mwisho wake kuwakamata wahusika wote yaani Lwakatare, yule aliyekuwa anahojiana naye, na wale ambao walikuwa wameamua kuufadhili mpango huo.
Endapo utakuwepo ushahidi wowote wenye kuonesha kuhusika ama moja kwa moja au kwa namna moja wamehusika, basi CHADEMA inapaswa ijichunguze yenyewe.
Kama Lwakatare alikuwa anapanga hayo akiwa anatekeleza amri au agizo kutoka kwa kiongozi yeyote wa chama basi kiongozi huyo akitajwa na ikithibitika mahakamani kuhusika kwake atapaswa kujiuzulu mara moja.
Kama video itaonekana kweli imechakachuliwa basi vyombo vya usalama vitatakiwa kutumia ari na nguvu ile ile waliyoitumia kwa Lwakatare kuitumia dhidi ya wahusika wa video hii kwani kuwaachilia, kuwapuuzia ni kukaribisha watu wengine kuanza kutengeneza makorokocho ya aina hii.
Lwakatare na Ludovick Joseph ambao walikamatwa katika tarehe tofauti mapema mwezi huu wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya ugaidi.
Katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao wanadaiwa kula njama kwa nia ya kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky kwa sumu, kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.
Katika shtaka la pili wanadaiwa kwa pamoja kula njama za kutaka kumteka Msacky na katika shitaka la tatu wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi.
Katika shtaka la nne linalomkabili Lwakatare peke yake ni la kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23 (a) cha kuzuia ugaidi nyumbani kwake.
Washitakiwa hao ambao wako mahabusu, huenda wakapewa dhamana leo wakati mahakama itakapokuwa ikitoa uamuzi wa kupewa dhamana au la.

1 comment:

  1. Pokies Pokies Online (Free) - KADangpintar
    Pokies Pokies. Games Available. Free Slots. Online Slots. Free Slots. Online Pokies Pokies. Pokies Pokies. 1xbet korean Free Slots. Free Slots. kadangpintar Online Pokies. deccasino Free Slots. Online Pokies

    ReplyDelete