Saturday, January 12, 2013

Tumechoka mgombea urais kuchaguliwa Dodoma



Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai

Na  Elias Msuya, Mwananchi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, kimeeleza nia yake ya kutaka kuachiwa mamlaka ya kumchagua mgombea urais wa visiwa hivyo, badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha wenzao wa Tanzania Bara.

Pamoja na hatua hiyo, chama hicho pia kinafikiria kurejea mtindo wa kupokezana kiti cha urais wa Tanzania kati ya bara na visiwani kama ilivyokuwa awali, ili kuweka usawa katika Muungano.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa huenda ikazua mpasuko na malumbano mapya kuhusu suala la urais ndani ya CCM, ambako harakati za baadhi ya wanachama wake wameanza kupiga mbio za kuutaka urais katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalumu visiwani humo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, alisema kwa sasa suala hilo linajadiliwa na kwamba ana matumaini kuwa litapatiwa ufumbuzi.

Hatua hiyo imekuja wakati Zanzibar ikiadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi yaliyoung’oa madarakani utawala wa mabavu wa Sultani, huku ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa Rais wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani, utakaofanyika 2015.

“Ndani ya CCM tuna utaratibu wetu wa kupata viongozi, lakini hilo suala la kuchaguliwa mgombea urais kutoka kwenye vikao vya Dodoma hata sisi limetugusa... Kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kulijadili ili tupate ufumbuzi,” alisema Vuai na kuongeza:

“Siyo tu kuchaguliwa mgombea urais, hata suala la kupokezana urais na jinsi ya kupata viongozi wengine kama wabunge na wawakilishi tunalijadili kwa kina. Ninaamini tutapata ufumbuzi… Siwezi kusema lini kwa kuwa chama chetu ni kikubwa mno, lakini tunalijadili.”

Vuai ametoa kauli hiyo, huku kukiwa na malalamiko ya Wazanzibari wengi kuhusu Muungano, ambapo wengine wanahoji iwapo kuna haja ya kuendelea na utaratibu wa sasa kupata mgombea na Rais wa Zanzibar ambao ni lazima upate baraka za CCM Bara.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema jambo hilo halijafikishwa kwenye vikao rasmi vya chama.

“Kama wao wanalifikiria hilo, acha waendelee, labda ungewauliza kama wameshalifikisha kwetu. Ukiniuliza mimi nitakujibu kuhusu utaratibu tulionao sasa, ila kama wao wana hoja nyingine, basi watazileta kwenye vikao husika zitajadiliwa,” alisema Nape.

Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, akizungumzia suala hilo alisema hayo ni maoni tu ya wananchi na wala Serikali haiwezi kuyaingilia.

“Wazanzibari wana haki ya kutoa maoni yao na wala Serikali hatuyaingilii. Lakini waelewe kwamba bado Muungano una faida kubwa kwetu. Hapa kwetu uchumi ni mdogo, ardhi ni ndogo pia Zanzibar inapata ulinzi na usalama kutoka kwenye Muungano,” alisema Waziri Aboud.

Mapinduzi na Muungano
Akizungumzia mafanikio ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Vuai alipinga madai kuwa Mapinduzi hayo yamemezwa na Serikali ya Muungano.
“Nakubali kuwa Mapinduzi yalilenga kuikomboa Zanzibar ili iwe huru, lakini siamini kama Zanzibar imemezwa na Muungano.,” alisema Vuai.
Hata hivyo, Vuai alikiri kuwa upo upungufu ya hapa na pale katika Muungano, ambayo yanapaswa kurekebishwa.

Kuhusu suala la Serikali mbili kama ulivyo msimamo wa CCM, Vuai aliuunga mkono utaratibu huo akisema kuwa Muungano unawasadia Wazanzibari katika ulinzi na usalama wao na kulinda umoja wa Watanzania wote.

Huku akiponda utaratibu wa Serikali tatu na Serikali ya mkataba kama inavyonadiwa na vyama vya upinzani, Vuai alisema bila Serikali mbili, Muungano lazima uvunjike.
“Muungano wa Serikali mbili ndiyo njia pekee ya kulinda umoja wa Watanzania. Serikali za mkataba zitavunja Muungano tu.,” alisema na kuongeza:

“Hizo Serikali tatu zitakuwa na michango kwa Serikali ya Muungano. Itafika mahali kila Serikali itatoa kisingizio, mara bei ya pamba, korosho imeshuka. Mara utasikia Zanzibar nayo inasema kuwa bei ya karafuu imeshuka, mara machafuko na mengineyo, mwisho Muungano utavunjika.”

Awaonya Wapemba
Vuai amewaonya wananchi wenye asili ya Pemba akisema wao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kutaka kuvunja Muungano na kuongeza kuwa endapo utavunjika ni wazi kwamba chokochoko hazitaishia hapo.

No comments:

Post a Comment