SAKATA la kupinga ujenzi wa bomba la gesi inayovunwa katika Kijiji cha
Msimbati mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, limechukua sura mpya baada ya
maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara kujiandikisha katika fomu maalumu kupinga
mradi huo.
Tayari majina hayo yamekabidhiwa kwa Katibu wa Wabunge wa Chama cha Wananchi
(CUF), Magdalena Sakaya kwa ajili ya kuyawasilisha bungeni kama kielelezo
halali cha wananchi hao kupinga mradi huo, ambapo utaratibu wa wananchi hao kujiorodhesha
uliandaliwa na chama hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa zaidi ya wakazi 30,000 wa Mtwara wamejiorodhesha
kupinga mradi huo wa gesi.
Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika
katika Viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi
kutoka wilaya zote tano ya mkoa huo, ambao hawakujali mvua kubwa iliyokuwa
ikinyesha.
Watu wa kada mbalimbali walisema kwamba haijawahi
kutokea umati mkubwa wa watu kuhudhuria mkutano wa hadhara mkoani humo kama
ilivyokuwa kwa mkutano wa jana.
Walisema kuwa idadi hiyo ya watu ni zaidi ya waliojitokeza katika maandamano ya kupinga mradi huo, yaliyofanyika Desemba 27 mwaka jana.
Walisema kuwa idadi hiyo ya watu ni zaidi ya waliojitokeza katika maandamano ya kupinga mradi huo, yaliyofanyika Desemba 27 mwaka jana.
Majina hayo yalikabidhiwa na makatibu wa CUF wa wilaya za mkoani huo
huku mwakilishi wao Saidi Kulaga, akisema kuwa zaidi ya watu 30,000
wamejiandikisha kupinga mradi huo.
Alisema wananchi hao wanataka Serikali kujenga mitambo ya kufua umeme
mkoani humo, ili kuinua uchumi wa mikoa ya kusini.
“Kwa niaba ya wananchi hawa na mbele yao, nakukabidhi majina na
sahihi zao, wakipinga mradi wa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam. Wazee
wetu waliwaondoa wanyonyaji weupe, sasa ni zamu ya vijana kuwaondoa wanyonyaji
weusi,” alisema Kulaga huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akipokea fomu hizo, Sakaya alisema kuwa wabunge wa CUF, wamesikia kilio cha
wananchi wa Mtwara na kwamba watahakikisha wanawasilisha katika Bunge lijalo.
Katika mkutano huo mabango kadhaa yalibebwa na baadhi yakisomeka: “Shemejiii
gesi haitoki…: Kikwete tuachie gesi yetu.”
Kabla ya mkutano kuanza umeme ulikatika eneo hilo hali iliyosababisha
kundi la vijana kuivamia Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mkoani
humo wakiishinikiza urudishwe, kitendo kilichowalazimu polisi kuingilia kati na
kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi hao.
Wananchi waliondoka eneo la ofisi hizo na kurudi uwanja wa mkutano, ambapo
baadaye na mkutano huo uliendelea kwa amani na utulivu, huku polisi
wakiwa katika tahadhari kubwa.
Kabla ya kutoa hotuba yake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro
aliwalisha kiapo viongozi na wananchi waliohudhuria mkutano huo, kikiwataka
kutorudi nyuma na kudai gesi hadi mwisho.
“Katibu wa wabunge na wabunge wote wa CUF, nawaagiza hakikisheni hoja hii ya
wananchi mnaifikisha bungeni na kuitetea, vinginevyo chama
hakitawaelewa,”alisema Mtatiro.
Tukio hilo linatokea wakati jana Waislamu walifanya dua maalumu ya kumwomba
Mwenyezi Mungu kutia wepesi hoja yao ya kutaka gesi ibaki Mtwara na kuwalaani
wale wote wanaotaka rasilimali hiyo iondoke.
Hata hivyo, katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa CUF, Katani
Katani alitoa taarifa kwamba moja ya gari lililokuwa limebeba wananchi kutoka
Tandahimba kwenda kwenye mkutano huo limepinduka na watu kadhaa wamejeruhiwa.
Katika siku za karibuni, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na taasisi
mbalimbali wamekuwa wakizungumzia suala la gesi, huku wakishinikiza wananchi
kuwa wasikubali gesi hiyo isafirishwe kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na
baadaye mikoa mingine.
Hatua hiyo ilisababisha kufanyika maandamano Desemba 27, mwaka jana
yaliandaliwa na kupokewa na viongozi wa vyama tisa vya upinzani na asasi kadhaa
zisizo za kiserikali yalikuwa na mabango kadhaa yenye ujumbe wa kupinga hatua
hiyo ya Serikali kusafirisha gesi hiyo.
Akizungumza wakati alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini, anayemaliza
muda wake Dianne Corner aliyekwenda Ikulu Januari 15 kumuaga, Rais Jakaya
Kikwete alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia rasilimali za
taifa, ikiwamo gesi asilia kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha
wananchi.
Baada ya maandamano hayo ya Desemba 27,2012, Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo alisema: “Nina wasiwasi na elimu ya hawa wanaoshabikia
hii gesi bila kufahamu. Ninawataka kwanza warudi tena shuleni, wanachokifanya
kuchochea wananchi na wananchi wanachofanya ni upuuzi tu.”
No comments:
Post a Comment