Sunday, January 20, 2013

Viongozi wamiminika kumwona Manumba

Afisa Mwandamizi Mtaafu wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambo (katikati) akiwa na Mtoto wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba,  Masanja Manumba (kulia) akiwa Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam jana.

VIONGOZI mbalimbali wa kitaifa wameendelea kufika katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam ili kumjulia hali Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, ambaye amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).
Mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, Ofisa Mwandamizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambow ni miongoni mwa viongozi ambao walifika hospitalini hapo jana na kupata fursa ya kumwona Manumba, wakati juzi Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilali naye alimtembelea.
Viongozi wengine ambao wamemtembelea Manumba ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na mke wake, Mama Salma Kikwete.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu wake Pereira Silima, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, Mkuu waJeshi la Polisi nchini, Said Mwema pamoja na maofisa wengine wa vyeo vya juu wa jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa Hospitali ya Aga Khan, imeeleza kuwa DCI Manumba bado anaendelea kutibiwa akiwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.
“Uongozi wa Hospitali ya Aga Khan unapenda kuujulisha umma kwamba Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, (DCI) Robert Manumba bado yupo hospitalini, ambapo anaendelea kupatiwa matibabu.
“Hali ya afya yake bado inahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Jaffer Dharsee alisema kwamba kesho atazungumzia kwa kina kuhusu matatizo yanayomsumbua Manumba hasa baada ya majibu ya vipimo alivyofanyiwa juzi na jana.
Dk Dharsee alithibitisha kubaini kuwa Manumba anasumbuliwa na malaria kali baada ya kumfanyia uchunguzi, ambapo baada ya kupatiwa huduma ya matibabu ya awali hali yake ilianza kutoa faraja. Ilielezwa kuwa kutokana na Manumba kutojitambua imeshindikana kumsafirisha kwenda kutibiwa nje ya nchi ingawa haikutajwa ni nchi gani ambayo angepelekwa kwa matibabu ya uhakika ili kunusuru uhai wake.

No comments:

Post a Comment