Walimu wa shule za
msingi katika wilaya ya magu mkoani Mwanza,wamekuwa wakitoroka katika vituo
vyao vya kazi na kuacha kufundisha kwa kuogopa kukamatwa kutokana na madeni
yanayotokana na kukopa kutoka kwa watu binafsi.
Hayo yameelezwa juzi (16/01/2013)na
Ofisa Elimu wa shule za msingi wilayani Magu, Yesse Kanyuma kwenye kikao cha
kazi cha viongozi wa elimu wa wilaya,waratibu elimu kata, walimu wakuu na
walimu wakuu wasaidizi kilichofanyika ukumbi wa CCM Mjini Magu.
Kanyuma alisema kuwa
baadhi ya walimu wilayani hapa, wameshindwa kufundisha na wamekuwa wakitoroka
kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kudaiwa na wakopeshaji hao ambao
wamekuwa wakichukua kadi zao za ATM za benki kwa makubaliano ya kulipa
mkopo kwa riba ya asilimia 50 mpaka 100,
kiwango ambacho ni kikubwa mno.
Alisema kuwa, kutokana
na hali hiyo kiwango cha taaluma katika shule zao kimeshuka sana, na kwamba
baadhi ya walimu anaodaiwa na watu hao wameshitakiwa mahakamani kwani
wameandikiwa mikataba na wakopeshaji hao ambao sio rasmi kisheria.
Aidha, wakati kikao
hicho kikiendelea, walimu wawili waliletewa barua za wito mahakani kutokana na
kushindwa kulipa kwa wakati mikopo waliyokopeshwa na wakopeshaji hao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa wilaya ya Magu, Bi Naomi Nnko amekemea tabia ya utoro wa walimu na
wanafunzi katika shule za wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment