Mshirika wa
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa
Ponda, katika kesi ya uvamizi wa eneo la ardhi, Maulid Namdeka
amewatupia tuhuma polisi waliowakamata kuwa walitaka kuwaua kwa kuwapiga
risasi ndani ya msikiti. Namdeka ambaye ni
mshtakiwa wa 38 katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Viktoria
Nongwa, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa tuhuma hizo jana
wakati akijitetea akiongozwa na Wakili wake, Juma Nassoro.
Pia, mshtakiwa huyo alikiri kufikia
eneo Markaz Chang’ombe kwa ajili ya kushiriki kujenga msikiti, baada ya
kutangaziwa na Imamu wa Mskiti wa Yombo kuwa, Waislam wanatakiwa kwenda
kushiriki ujenzi wa mskiti huo.
Katika ushidi
wake, Namdeka alidai kuwa alifika eneo hilo Oktoba 16, mwaka jana kwa
lengo la kushiriki Ibada ya Itikafu na ujenzi wa msikiti huo kesho yake.
Hata hivyo,
alidai usiku wakiwa kwenye ibada, walivamiwa na polisi na kwamba
kiongozi wa polisi hao aliwaamrisha askari wake wawapige risasi
msikitini, lakini askari mmoja alipinga kuwa hawawezi kuwapiga risasi
kwa sababu hawana silaha.
Namdeka ambaye
alitoa ushahidi huo wa utetezi akiwa shahidi wa 30 upande wa utetezi,
alidai baada ya hapo walikamatwa wote na kupelekwa Kituo cha Polisi
Mabatini, Kijitonyama.
Tofauti na
washtakiwa wengine waliokwishatoa utetezi, wakati akihojiwa na Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, Namdeka alikiri kutoa maelezo ya
onyo yaliyoandikwa na askari mmoja kuhusiana na tuhuma za uvamizi wa
eneo hilo.
Habari -
James Magai, Mwananchi
Chanzo -
Mwananchi
No comments:
Post a Comment