Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo
haja kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
kufikiria upya uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012
na kutaka itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.
Akizungumza na waandishi wa habari Jana mchana, mara baada
ya kikao cha Kamati ya Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu
jambo hilo likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk.
Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.
Rais wa TFF anayemaliza muda wake Reodiger Chilla Tenga akizungumza na waandishi wa Habari hivi karibuni |
“Kamati ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa
Waziri hata kidogo, ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake,
athari zake na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri
vibaya,” amesema Rais Tenga.
Amesema rai ya TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni
kitu gani wafanye kunusuru mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo
hili litakwisha baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya
kufanya uamuzi huo hakuwasikiliza.
Katika mkutano huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF
inaiheshimu sana Serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri,
lakini akaongeza kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.
Amesema lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini
migongano ya maagizo hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana
na maagizo hayo.
Rais Tenga amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo
wanachama wake ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina
taratibu za kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake
ambazo zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo
vimeunganishwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu
na kufuata maagizo na miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa
miguu.
Rais Tenga amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi
na uendeshaji wake, kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF,
na madhara yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama
wake katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya TFF.
“Sheria za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama
kamili kinatakiwa kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya
kuanzishwa kwake. Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na
gofu, hapo Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.
Kuhusu maagizo ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11
cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama,
na si marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo
ameongeza kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.
“Ukienda kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza.
TFF tulipowasilisha marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema
sawa. Jambo la kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya jambo
hili kufikiriwa upya.
“Usajili tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu,
mwathirika anakuwaje TFF? Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,”
amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo
ndiyo Waziri ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.
Akizungumzia historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais
Tenga amesema ni zao za Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini
na kugongwa mhuri na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo
ndiyo iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.
“Huko ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa
Katiba ya 2004. Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya
Waziri yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana
na ridhaa ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna nafasi
ya BMT,” amesema.
Amesema katika maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata
Katiba ya 2006 na kanuni za BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi
ya BMT, na hata kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.
“Kwa maagizo haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya.
Tunajua hakuwepo katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya
Serikali na FIFA kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.
Pia amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna
marekebisho mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta
maana yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya
Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi,
Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.
“Kwa uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri
sidhani kama alikuwa anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua
asingefanya uamuzi huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa
Katiba ya 2006 unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa
vile vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.
Amesema kwa Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi
wa TFF ambapo madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza
mpira, klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa
pembeni kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.
“Dhana kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio
nje ya mpira wa miguu. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza
tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki hivyo,
kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.
“Nia yetu bado ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,”
amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi
la TFF kwa Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.
“FIFA wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo
utaheshimika. Kama mtu wa mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni
kuhakikisha watu wanapewa haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo
maana FIFA wanakuja,” amesema.
Akijibu swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho
ya Katiba hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya
marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono na 33
walikataa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment