Monday, May 27, 2013

KITUO CHA MABASI MAGU KIWE NA CHOO BORA

Magu ni Wilaya Yetu, Magu ni Kwetu.


Haya ni Mazingira ya Stand Magu


Pengine haya siyo mazingira mageni kwako kama ni Mwanamagu. Lakini la msingi sana ni Taswira ya Mji wetu wa Magu. Taswira ya mji wowote hapa nchi kwetu ni mazingira ya safi hasa ya kituo cha mabasi au stand ambapo ndipo wageni wengi hufikia kabla ya kuingia maeneo mengine ya Mji. 


Hiki ni choo cha Kulipia Magu
 
Vituo vingi vya mabasi maarufu kama Bus Stand vilivyopo kote nchini havina budi kuwa na vyoo bora ikiwa ni pamoja na mazingira ya vituo hivyo kuwa safi wakati wote. Hii inatokana na ukweli kwamba wasafiri wengi wanaotoka maeneo mbalimbali wanaopita kwenye vituo hivyo inawalazimu watumie vyoo kwa ajili ya haja ndogo au kubwa.


Mazingira ya Nje Choo cha Magu Bus Stand


Wakati huo huo, katika vituo vingi vya mabasi, vinauzwa vyakula na vinywaji mbalimbali, kwa maana ya vile vya migahawani na vyakula vinavyouzwa na wafanyabiashara wadogo wadogo mikononi. Kutokana na fursa hii, ni dhahiri kuwa wasafiri wengi wanaopita kwenye kituo cha mabasi Magu, ambao wengi wao ni Watanzania wenzetu, inawalazimu kutumia vyoo ili kukidhi haja walizokuwa nazo.


Kwa maana hiyo vituo vingi vya mabasi hapa nchini vimejengwa kwa minajili ya kuwa na vyoo ili kuwafanya wasafiri, wasipate taabu pale watakapojisikia kushikwa na haja ya kutembelea vyooni. Kwa mfano ukitembelea baadhi ya Wilaya Tanzania hii, utajionea sehemu nyingi zenye mazingira mazuri na masafi ya vyoo.Wilaya ya Nyamagana, Same, Nzega, Maswa kwa kutaja chache wako juu sana kwenye suala la usafi wa vyoo.






Haya ni Matenki ya Kuhifadhia Maji ambayo hata hivyo hayatoshi


Katika Wilaya yetu ya Magu, yaani Magu Stand kuna choo kimoja ambacho hali yake ya usafi hairidhishi kabisa. Pamoja na ukweli kwamba wasafiri wengi sana hupitiia kwenye kituo hiki, tatizo linakuja pale abiria au msafiri, anaposhikwa na haja, inabidi aende msalani lakini kwa shingo upande.

Ni haki ya wanamagu, watanzania na wasafiri wote wanaopita Magu Stand kuwekewa mazingira safi ya choo ikiwemo kuwepo kwa maji ya kutosha ili kuwafanya wajisikie huru, pindi haja zitakapo washika wanapokuwa safarini au kwa wale wanaoshinda wakifanya shughuli zao mbalimbali pale Stand.




Choo cha Magu kinavyoonekana kwa Nje


Kwa upande mwingine, kwa kuwa vyoo hivi vimepewa watu binafsi kuviendesha au kusimamia, basi watu hao wana wajibu wa kuvitunza kwa kuvisafisha kiukweli kabisa ili uchafu unaoonekana kung’ang’ania kwenye kuta uondoke na kuacha mazingira safi. Ni aibu kuwa mkusanya pesa pekee badala ya kukusanya sehemu ya pesa hiyo wakati huo ukiwekeza kwenye usafi wa choo chenyewe.

Hali kadhalika kutokana na umuhimu huo, halmashauri ya wilaya ya Magu, inastahili kubeba lawama kwa upande mwingine kutokana na ulegevu wao katika kulisimamia hili.

Maji safi na salama ndilo tatizo kuu hasa kuhusu upaikanaji wake. Mapendekezo ya watu wa afya ni kuwa ni lazima kuwe na vyanzo vya kutosha vya maji kwa kuwa maji mengi sana hutumika kusafirisha vinyesi na mkojo. Kwa hiyo kwa vyovyote vile ni lazima kuwe na vihifadhio vya maji ya kutosha ili kuwezesha kukusanya maji ya kutosha kwa kazi hiyo.




Hii ni chema katika choo hicho




Utupaji wa kinyesi ulio salama kama kanuni za afya zinavyoelekeza huweza kusaidia kujikinga na maradhi mbalimbali ya kuambukiza na ya milipuko ambayo husababishwa na vimelea vinavyosababisha maradhi hayo, vikitokea kwenye kinyesi au mkojo.

Magonjwa hayo ambayo wanamagu, watanzania na wasafiri wanaweza kuyapata kutokana na hali hiyo ni pamoja na yale yanayosababishwa na bakteria, kama vile kipindupindu, typhoid, kuhara, kuhara damu, na mengine. 

Pia kuna yanayosababishwa na virusi kama vile kupooza (Poliomyelitis), yapo pia yanayosababishwa na protozoa kama Amoeba na mwisho ni yale ya minyoo mbalimbali na kichocho. Hivyo utupaji wa kinyesi unaofuata kanuni za afya ni wa muhimu sana ili kuwalinda wanamagu wote hasa wanaotumia vyoo hivyo.

Uchafu wa mazingira kwenye kituo chetu cha basi cha Magu utatusababishia magonjwa katika jamii, ili kuepuka uchafuzi wa mazingira kwenye kituo hatuna budi kuzingatia, misingi ya afya binafsi, usafi wa mazingira na, kuhakikisha uchafu hauzagai ovyo.


Sehemu ya kujisaidia haja ndogo(Mkojo)





Hii ni sehemu ya kuosha mikono ambayo nayo haina muonekano wa usafi chooni hapo



Hii ni sehemu ya kujisaidia haka kubwa (Kinyesi) ya choo cha Magu Bus Stand

Taasisi husika zikishirikiana na vyombo vya habari vichukue jukumu la kuelimisha wasimamizi na watumiaji wakubwa wa vyoo hasa pale wilayani ili kuwahamasisha na kushirikiana na jamii katika masuala ya usafi wa mazingira yote ya Stand Magu.

Ikumbukwe kwamba kinga ni bora kuliko tiba, hivyo juhudi za makusudi hazina budi kufanywa ili kuondosha kabisa tatizo hili lenye athari kubwa ki afya na mazingira kwa ujumla. Tukiamua tunaweza kabisa kufanikisha hili, wala hatuhitaji mjomba toka nje.

“Pamoja Tunajenga Magu yenye Maendeleo Endelevu”

No comments:

Post a Comment