Thursday, March 21, 2013

UHAMIAJI MKOA WA MWANZA YANASA WATATU.

IDARA ya Uhamiaji Mkoani Mwanza imeendelea kuwanasa Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa njia za panya baada ya hivi karibuni kuwakamata vijana watatu raia wa Burundi.

Akizungumza ofisini kwake leo Naibu Kamishina Msaidizi na Kaimu Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza Bi. Anamaria Yondani alisema kwamba hii inatokana na Idara hiyo kuendelea kupokea taarifa kutoka kwa wananchi na kuzifanyia kazi, huku pia uhamiaji ikiendelea kutekeleza mradi wa Shirika la Kimataifa ambalo linahusika na shughuli za Kiuhamiaji (OIM) kupitia mradi wa Capacity Buiding in Migration Management (CBMM-II)

Bi Yondani aliwataja vijana hao waliokamatwa kuwa ni Akizmana Adamu (15), Gerlad Michael (17) na Boaz Ernest (15) wote wakazi wa Ruingi  raia wa nchi yaBurundi walioingia nchini kwa njia za Panya kupitia Mkoani Kigoma kabla ya kunaswa Mkoani Mwanza wakiwa kwenye harakati za kutafuta kazi ili kuwasaidia kuishi nchini kinyume cha taratibu na sheria za nchi.

Kaimu Mkuu huyo wa Uhamiaji Mkoa  alisema tatizo la wahamiaji haramu limekuwa ni Janga la Kitaifa na Mkoa wa Mwanza ni Kitovu cha Mawasiliano, Biashara ,Elimu na Usafiri kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nchi za Maziwa Makuu na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akitoa taarifa ya Mkutano wa Kamati ya  National Immigration Inter-regional Steering Committee (NIISC) uliofanyika Mjini Sumbawanga Mkoani Rukwa Machi 11 hadi 12 mwaka kwa lengo la kuendeleza mradi wa CBMM-II, kuongeza Mikoa wanachama wa NIISC na Namna ya kushirikiana na IOM katika kuendeleza mradi wa huo ambayo yalijadiliwa katika mkutano huo.

“Mradi huu wa NIISC awali ulianzisha na Mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Kigoma mwaka 2012 na kasha kuongeza Mkoa wa Rukwaa hii ikumbukwe ipo katika Kanda ya Ziwa ambapo kuna vivutio  kadhaa vinavyosababisha wahamiaji haramu kuingia na kujipenyeza katika sekta za i Uvuvi, Kilimo, Ufugaji, Madini, Biashara, Elimu na Usafiri  hali ambayo Uhamiaji imekuwa ikizifanyia  doriawavutia ”alisema

Aidha katika mkutano huo  uliweza kuongeza wanachama wapya katika Kamati ya NIISC ambayo ni Mikoa ya Geita, Shinyanga ,Tabora na Katavi ili kuongeza ushirikiano katika kubadilishana taarifa na uzoefu wa utekelezaji wa majukumu ndaji ya kila siku katika kupambana na wimbi kubwa la wahamiaji haramu.

“Tunatambua wahamiaji haramu bado wanaendelea kupitia  nchini mwetu kwa ajili ya kuelekea  nchini Afrika ya Kusini ambapo awali walikuwa wakipita Mpaka wa Sirali kutokea nchi ya Kenya kuingia Wilaya ya Tarime,Musoma kisha Mkoani Mwanza na kuelekea Mikoa ya Kati hadi Mkoani Mbeya kabula ya kuanza safari kuelekea nchi za kusini hadi Afrika Kusini ili kuwa lahisishia kwenda nchi za Ulaya”alisema.

Bi Yondani alisema kwamba baada ya kutekelezwa kwa mradi wa CBMM-II wahamiaji haramu  waliamua kubadili njia pengine kupita mawakala ambao ni raia wa Tanzani wanaowasaidia kuwaingiza kwa njia haramu na sasa kupitia Mikoa ya Kaskazini ya Kilimanjaro,Arusha,Manyara na Tanga na kuelekea mikoa ya Kati kwa ajili nya kuelekea Mkoani Mbeya na kuvuka kuelekea Malawi na Zambia.

“Lengo kuu la wahamiaji haramu ni kwenda Afrika Kusini ni kutafuta maisha bora na kuwa njia lahisi ya kwenda Mataifa ya Bara la Ulaya na Marekani huku wahamiaji wengi wanaoingia kinyume na utaratibu wa kisheria wengi ni kutoka nchi za Ethiopia,Eritrea na Somaliaambao wamekuwa wakinyanyaswa, kuteswa na kufariki wanapokuwa safarini kwenye maroli ya mizigo na watu wanaowasaidia”alisema

“Wanatumia njia za panya kusafiri kupita mipaka isiyo rasimi  na husaidiwa na mawakala  (Maajenti) wao ambao wengine ni watanzania wasio na uzalendo na wamekuwa wakiwapakiza katika maroli ya mizigo,magari ya makontena  na hata wengine kupitishwa kwenye Hifadhi za wanyama wakali na baadhi yao kupitia Ziwa Victoria kwa mitumbwi na kuvuka mito yenye wanyama wakali wakati wa usiku”alieleza

Bi.Yondani ametoa wito kwa wananchi kurejesha uzalendo wa Taifa na kushirikiana na maafisa uhamiaji na polisi kutoa taarifa kwa watu ambao wanawahisi kuwa siyo raia na watu ambao wameingia kwa njia za panya katika maeneo mbalimbali ya Mikoa yao na wanaotafuta kujipenyeza kufanya kazi ambazo zitawasaidia kuonekana kuwa ni raia wakati huu taifa linaelekea kutoa vitambulisho vya uraia .

“Wananchi sasa warudishe uzalendo wao na kuacha kuwasaidia wageni na wahamiaji haramu walioingia nchini kinyume cha taratibu na kuvunja sheria za nchi kwa kuwatolea taarifa kwa ofisi za uhamiaji na vituo vya jeshi la polisi kwa lengo la kupambana na janga hili la kitaifa la kupambanana wahamiaji haramu wanaoingia nchini kila siku kwa kusaidiwa na mawakala na kuhifadhiwa na watu wasiokuwa na uzalendo”alisisitiza

Amevipongeza vyombo vya habari kwa kushirikiana na Idara hiyo kutoa taarifa kwa wananchi ikiwemo Elimu kwa kueleza bayana athari za kuwa na wahamiaji haramu ambao wengi wao wamekuwa wakifanya uhalifu na kuwapora mali na kufanya mauaji kwa wananchi na sasa wananchi katika maeneo yao ya mitaa na kata kuwa kuwatolea watu ambao si raia ili kuwabaini kabla ya kutolewa vitambulisho vya uraia kitaifa.

Taarifa Rasmi kutoka Wizara ya Ujenzi: Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imewafukuza Kazi na kusitisha Mikataba ya Wafanyakazi waandamizi Saba wa Wizara na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa tuhuma za ubadhilifu na Utendaji kazi Mbovu.



Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imewafukuza kazi na kusitisha mikataba ya Wafanyakazi Waandamizi saba wa Wizara na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa tuhuma za ubadhirifu na utendaji kazi mbovu.

 Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Wizara ya Ujenzi ya kusafisha Wakala zake na  kuongeza ufanisi.

Katika nyakati tofauti Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akipokea tuhuma za vitendo vya ubadhirifu miongoni mwa watendaji waandamizi katika Wakala zinazotoa huduma chini ya wizara hii.

Kufuatia tuhuma hizo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi maalum katika ofisi za  TBA Mkoa wa Dar es salaam na Katibu Mkuu wa wizara Balozi Herbert E. Mrango na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Elius Mwakalinga waliunda Kamati za kupitia taarifa za CAG na taarifa nyingine.

Kamati hizo zimeweza kubaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za fedha, manunuzi na uendeshaji.

Maafisa waliofukuzwa kazi ni pamoja na Bw. Charles Gabriel Lyatuu ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam; Bw. Ladislaus I. Kapongo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam) na Bi. Agness F. Chambo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam).

Aidha, kwa Mkurugenzi wa Biashara na Fedha Bibi Yona Orida na Injinia Charles Makungu ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Miliki wameondolewa katika nafasi za uongozi  walizokuwa nazo TBA.

Hatua zaidi zilizochukukuliwa ni kuwashusha vyeo Meneja wa Mkoa wa Pwani Bibi Esteria M. Nyamhanga na Bw. Samwel C. Samike ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa Mbeya.

Hatua hizi zimechukuliwa kunatokana na watendaji hao kuhusishwa na tuhuma za ubadhidilifu ambazo zimebainika kufanyika katika taasisi hiyo. Maeneo ambayo yamebainika kuwa na ukiukwaji mkubwa ni pamoja na kufanya malipo kwa kutumia mikataba isiyosainiwa na pande zote,  kufanyika malipo kinyume na taratibu za manunuzi na hata malipo kufanyika kwa fedha taslim kinyume na taratibu.

Aidha, eneo la manunuzi ya viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya TBA pia yameonyesha kuwa na vitendo vya ubadhilifu na ukiukwaji wa taratibu.  Vipo viwanja vilivyobainika kununuliwa nje ya taratibu, baadhi ya nyaraka kuonyesha ukubwa tofauti na ule uliolipiwa, kununua maeneo yasiyofaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Serikali, kuongeza bei na kufanyika kwa malipo kabla ya mikataba kusainiwa.

Hatua zilizochukuliwa ni muendelezo wa juhudi za Wizara za kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayoashiria kuwa na utendaji ulio nje ya maadili yanafuatiliwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Aidha, ili kuboresha ufanisi katika Wakala hivi karibuni waliteuliwa Mameneja wapya 15 wa TEMESA katika mikoa mbali mbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwahamisha vituo mameneja wengine.

 Kwa upande mwingine, ajira za Watendaji katika vituo vyote vya mizani tayari zimetangazwa na kwa sasa kazi ya kupitia maombi yaliyowasilishwa inakamilishwa ili kuhakikisha kuwa watendaji wasio waaminifu hawapati nafasi katika maeneo hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa vitendo vya ubadhirifu.

Wizara itaendelea kuchukua hatua za aina hii pale ukiukwaji wa sheria na taratibu za utumishi wa umma utakapobainika.

Taarifa hii imetolewa na;

M.S. Ntemo

MSEMAJI WA WIZARA YA UJENZI

Wednesday, March 20, 2013

Ikulu, wizara watofautiana hatua dhidi ya kigogo wa Itifaki

Ikulu imetoa kauli inayopingana na ile ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu hatima ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Itifaki cha wizara hiyo Anthony Itatiro, ambaye anatuhumiwa pamoja na maofisa wengine wa wizara hiyo kupanga njama ya kuchota Sh3 bilioni baada ya kubuni safari feki ya Rais.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
 
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alimwambia mwandishi wa habari hii jana kuwa Serikali imeshachukua hatua za kinidhamu dhidi ya Itatiro kwa kumvua hadhi ya ubalozi na kutenguliwa nafasi yake ya ukurugenzi wa Itifaki.
Hata hivyo, kauli ya Sefue ambaye ndiye Mkuu wa Utumishi serikalini, inapingana na ile iliyotolewa juzi na Naibu Waziri katika wizara hiyo, Juma Mahadhi ambaye alikaririwa akisema kwamba Itatiro bado yuko kazini na kwamba suala lake lilikuwa likisubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete.
Mahadhi alitoa kauli hiyo alipobanwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli aliyehoji hatima ya tuhuma hizo wakati wa kikao cha kamati hiyo.
Hata hivyo, jana Sefue akizungumza na Mwandishi wa habari hizi alisema: “Uteuzi wake umetenguliwa baada ya kutokea hilo tatizo, hatua ya kinidhamu tuliyomchukulia ni kumwondoa katika nafasi hiyo pia hata ule wadhifa wake wa ubalozi pia tumemwondolea.”
Sefue alisema nafasi ya Mkuu wa Itifaki iliyokuwa ikishikiliwa na Itatiro hivi sasa anakaimu mtu aliyemtaja kuwa ni Andi Mwandemba na kwamba hatua hizo zimechukuliwa mwaka huu, lakini akasema hakumbuki tarehe.
Alipoulizwa hatua zaidi ambazo atachukuliwa kigogo huyo alijibu; “Itatiro atatafutiwa kazi nyingine ambayo ni ya chini zaidi kuliko aliyokuwa nayo awali, yaani cheo cha chini kuliko alichokuwa nacho.”
Sefue alieleza kuwa utaratibu uko wazi kwamba linapogundulika jambo ambalo siyo la kawaida hatua za kinidhamu ni lazima zichukuliwe.
“Inapogundulika kuwa mambo hayaendi vizuri hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe ili iwe funzo kwa wengine,” aliongeza Sefue, ambaye ni Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
Alipoulizwa kama ni hatua stahili kwa kumvua wadhifa mtu anayehusishwa katika njama za kutaka kuchota kiasi cha Sh3 bilioni, alijibu kuwa hiyo ni hatua ya kinidhamu na pia ni fundisho kwa wengine.
Kauli ya Mahadhi
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alimhoji Mahadhi kuhusu jaribio la wizi lililofanywa na maofisa wa wizara yake baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam juzi.

Mahadhi alisema wizara ilichukuahatua dhidi ya maofisa wa ngazi za chini wakati suala la Itatiro lilikuwa mikononi mwa Rais Kikwete kutokana na wadhifa wake.
Naibu waziri huyo alidai walichukua hatua hiyo kufuatia ushauri waliopewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi wa Ndani walioendesha uchunguzi wa njama hiyo.

“Takukuru na mkaguzi waliona hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao na ndiyo wakashauri wachukuliwe hatua kali za kinidhamu,” alisema Mahadhi.

Itatiro na maofisa wanne wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walituhumiwa mwaka jana kupanga njama za kuchota kiasi hicho cha fedha bila ya kuwapo kwa ziara ya Rais kwenda nchi yoyote ya kigeni.
Mpango huo unadaiwa kusukwa Juni mwaka jana kwa maofisa hao kwa kuitaka Wizara ya Fedha kutoa kiasi hicho cha fedha.

Wasimamizi afya ya uzazi wapatiwa kompyuta

SHIRIKA lisilo la kiserikali Tandabui Health Access Tanzania (THAT)/Afya radio la jijini Mwanza limekabidhi kompyuta nne zenye thamani ya sh milioni 4.4 kwa wasimamizi wa huduma ya afya ya uzazi mkoa wa Mwanza na wilaya ya Ilemela, Geita na Nyamagana, ili kuboresha huduma hiyo.
Akikabidhi kompyuta hizo kwa mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, waganga wakuu wa wilaya za Ilemela, Nyamagana na mratibu wa afya ya uzazi wilaya ya Geita, meneja miradi wa shirika hilo, Doto Biteko, alisema lengo la kutoa kompyuta hizo ni kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na wasimamizi hao katika kufikia upatikanaji wa huduma bora.
Alisema kompyuta hizo zimeunganishwa na mfumo wa mawasiliano wa shirika hilo unaoratibu ubora wa huduma zitolewazo kwa wajawazito kwenye vituo vya afya, ili kuwawezesha wasimamizi na waratibu hao kupata taarifa za moja kwa moja kutoka kwa wananchi.
Aliongeza kuwa mfumo huo unakusudia kuongeza kasi ya uwajibikaji wa wasimamizi wa huduma za afya hasa za mama na mtoto kutokana na taarifa za utolewaji wa huduma vituoni kuwafikia kwa muda muafaka na bila kuhaririwa.

TPSF yapongezwa kuimarisha sekta binafsi nchini

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepongezwa kwa jitihada inazochukua hivi sasa kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakuwa imara, sauti moja na hivyo kuchangia zaidi katika ujenzi wa uchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Mwanza hivi karibuni, Jovita Bubere na Moses Nyaronga, walisema TPSF imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara zao na kuongeza mitaji.
“Tunaomba taasisi hii iendelee na jitihada zake za kuwasaidia wanachama wake mikoani, ili kuendelea kutujenga katika kukuza biashara hasa kwa mikutano kama hii ya kikanda,” alisema Bubere wakati wa mkutano ulioshirikisha wanachama wa TPSF Kanda ya Ziwa.
Bubere ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya kinamama Wajasiriamali Tanzania, alisema: “Tunahitaji msaada mkubwa ili kuweza kufikia malengo yetu.”
Akizungumzia soko la Afrika Mashariki, mwenyekiti huyo alisema wamejipanga vizuri na tayari wameshaanza kutoa mafunzo kwa baadhi ya kinamama kuhusiana na mbinu za kutumia ushindani unaokuja wa kibiashara.
Kwa upande wake, Nyaronga ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la Lemon Development Foundation lililoko katika wilaya ya Rolya, mkoani Mara, alisema huu ndio wakati wa kuiunga mkono TPSF, ili iweze kufanya kazi kwa uhakika zaidi ya ilivyo sasa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Geofrey Simbeye, alisema taasisi hiyo ina lengo la kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wanachama wake katika kuongeza kasi ya uanzishwaji wa makampuni na viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira na kuinua uchumi wa nchi.

Wakulima A. Mashariki wahimizwa kuungana

RAIS wa Shirikisho la Wakulima wa Afrika Mashariki, Philip Kiriro, amewataka wakulima wadogo kuungana katika kupigania maslahi yao, ili kujikomboa kutoka kwenye ukulima mdogo hadi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kiriro alisema iwapo wakulima hao hawataungana mafanikio yao hayatakuwa mbali.
Alisema shirikisho hilo lenye makao makuu nchini Kenya, limekusudia kuwaunganisha wakulima kwa lengo la kuwa na sauti moja katika maamuzi yao ambapo litafanya kazi na serikari za nchi hizo.
“Tumekuja hapa nchini kukutana na Shirikisho la Vyama Ushirika, pia kutembelea ofisi za serikali na kuifahamisha serikali juu ya shirikisho hilo litakavyofanya kazi na wakulima wadogo katika nchi za Afrika Mashariki,” alisema Kiriro.
Aidha alisema kati ya nchi zilizopo kwenye jumuia hiyo, Tanzania ina fursa ya kufanya vizuri katika kilimo kutokana na kuwa na maeneo makubwa kwa shughuli za kilimo.
Naye Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TCC), Willings Mbogo, alisema watahakikisha kupitia shirikisho hilo wanakuza uwezo wa wakulima wadogo na wajasiriamali, ili waweze kukuza uchumi kutoka katika hali ya sasa na kuufanya uwe bora zaidi.