KATIBA




KATIBA YA UMOJA WA WANAMAGU 2009
MAGU DEVELOPMENT INITIATIVE (MDI)





TWIKOMIGE


2009


1.    UTANGULIZI

1.      MISINGI YA KATIBA
KWA KUWA SISI Wana -Magu rasmi na kwa dhati tumeamua kuungana kwa shughuli za maendeleo ikiwa kama msingi wa kujenga jamii inayozingatia uhuru, haki, udugu na amani,

NA KWA KUWA uhamasishaji wa shughuli za kiuchumi, jumuiya na urafiki miongonimwa wana Magu ni muhinu kwa maendeleo na ambayo inaweza kusaidia jamii kujua sehemu muhimu za maendeleo,

NA KWA KUWA Magu ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na watu wake ndiyo nguzo
na nguvu kazi kuu ya kuleta maendeleo Wilayani humo, na kutowajibika kwao katika shughuli za maendeleo au kwa mchango wowote ule, ni sawa na kutoliendeleza taifa zima la Tanzania,

KWA HIYO BASI, sisi kama wananchi wa Tanzania wazaliwa wa Magu tunaoishi Dar es salaam tumeamua kuungana na kuunda jumuiya ambayo itafuata katiba hii.

2.      TAFSIRI YA MANENO
Tafsiri ya maneno katika katiba hii ni kama ilivyoelezwa hapa chini isipokuwa pale itakaposemwa vinginevyo katika katiba hii:
Magu
Magu” Wilaya ya Magu ambayo ipo Mkoa wa Mwanza, Tanzania;

MDI
MDI” Magu Development Initiative (Jumuiya ya Uhamasishaji Maendeleo Magu) Ni kikundi cha hiari kilichoanzishwa kwa mujibu washeria na kanuni za Mashirika yasiyo ya kiserikali;

“TWIKOMIGE”
“TWIKOMIGE” Tuhimizane kuleta maendeleo;

“Katiba”
“Katiba” Mwongozo wa kanuni na sheria zinazolinda maslahi ya jumuiya na wanachama;

“Mfilisi”
“Mfilisi”   Taasisi iliyoteuliwa kusimamia mali za mashirika yanayovunjika au kufilisika;

“Mwanachama”
“Mwanachama” Mtu yeyote aliyetimiza masharti na kujiunga na Magu Development Initiatives (MDI);



2.    IBARA 1
1.     JINA LA JUMUIYA
Jumuiya itaitwa “Magu Development Initiative” (MDI/ TWIKOMIGE)
Jumuiya itakuwa ni ya hiari, isiyotengeneza faida, isiyo ya kiserikali na ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Mashirika yasiyo ya kiserikali

2.      MAKAO MAKUU
Makao Makuu ya asasi yatakuwa ni Dar es salaam Tanzania. Shughuli zote za umoja zitafanywa kwenye makao makuu ya umoja na sehemu zingine zozote kama itakavyosemwa katika katiba hii.

3.      LUGHA RASMI
Lugha zitakazotumika katika umoja zitakuwa ni Kiswahili na Kiingereza

4.      DIRA
Kuona jamii iliyohamasika na inayojishughulisha katika maendeleo ya watu wake, kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira, utamaduni na teknolojia endelevu.
3.    IBARA 2
1.     MALENGO YA JUMLA
Lengo la jumla la umoja huu litakuwa ni kuwaweka pamoja wananchi wote wa Wilaya ya Magu iliyoko Mkoa wa Mwanza Tanzania kwa dhumuni la Kuelemisha na kuhamasisha wananchi kuendeleza utamaduni na tabia ya kufanya kazi kwa ushirikikiano unaojenga uwezo wa kujitegemea na kuleta mabadiliko ya maisha bora kwa watu wote katika familia na jamii kwa ujumla ili kujenga amani, umoja, haki, udugu, demokrasia, elimu, uchumi, utawala bora, na mazingira nadhifu katika jamii.

2.     MALENGO MAHUSUSI
a)    Kufanya utafiti, kuhamasisha na kubaini changamoto mbalimbali za maendeleo zinazoikabili Wilaya ya Magu;
b)   Kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika huduma za awali za afya, uzuiaji wa magonjwa ya kuambukiza hususani UKIMWI, Kifua Kikuu nk;
c)    Kuwaandaa wanawake na wanaume wote kwa pamoja kukabiliana na maisha ya utandawazi hasa katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia endelevu;
d)   Kuhamasisha utunzanji wa mazingira hasa hifadhi na utunzanji maliasili (ardhi, uoto wa ardhi, ziwa, mito, milima nk) ili koboresha mazingira kwa maisha bora;
e)    Kusaidia na kubuni njia mbadala za kuwasaidia wale wote wasio jiweza hasa maskini, walemavu, yatima, watoto wa mitaani pamoja na makundi yote yanayohitaji misaada;
f)     Kuhamasisha na kufanya harambee mbalimbali kwa ajili ya kuboresha miradi ya jumuiya yetu;
g)   Kutoa elimu, habari mbalimbali kwa wanajumuiya na kuhamasisha ushrikiano;
h)   Kuhamasisha na kujenga uwezo wa makundi mbalimbali ya wanachama na jamii kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo na uzalishaji;
i)     Kupanua eneo la kiutendaji ili kuweza kuwafikia wana Magu wengi zaidi ambao wametawanyika kokote dunia;
j)     Kujenga mtandao wa ushirikiano na taasisi, makampuni, serikali, wafadhili na watu binafsi ili kubadilishana ujuzi, uzoefu katika harakati za maendeleo;
k)    Kuhamasisha na kushirikiana na jamii yote ya Watanzania kupambana na rushwa;
l)     Kuhamasisha na kuhakikisha usawa wa jinsia katika jamii kulingana na kanuni zinazosimamia maendeleo katika jamii yetu;

4.    IBARA 3
1.     UANACHAMA
Jumuiya yetu itakuwa na aina zifuatazo za wanachama:
a)      Kutakuwa na wanachama waasisi ambao watakuwa ni wale wote watakaokuwepo hadi siku ya mkutano wa mwisho kabla ya kusajili Umoja wetu. Wanachama hawa pia watatakiwa kulipa kiingilio kiasi cha shilingi 50,000/= na malipo ya mwezi ni kiasi cha shilingi 10,000/=.
b)      Kutakuwa na wanachama wa kawaida ambao watakuwa ni Watanzania wote wanaotoka katika Wilaya ya Magu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 55 ambao watakubaliwa kujiunga baada ya kulipa kiingilio kiasi cha shilingi 50,000/= na malipo ya mwezi kiasi cha shilingi 10,000/=.
c)      Kutakuwa na wanachama wa heshima ambao watakuwa ni Watanzania kutoka Magu wenye umri kuanzia miaka 56 na kuendelea lakini bado wanaunga mkono shughuli zote za jumuiya yetu na watatakiwa kulipa kiasi cha shilingi 50,000/= kama kiingilio na 10,000/= kama ada ya mwisho wa mwezi.
d)     Kutakuwa na wanachama washirika ambao watakuwa ni jumuiya mbalimbali ambazo zitakuwa zinatumia na kutegemea sera na kazi mbalimbali za jumuiya yetu na kutoa misaada ya kifedha. Jumiya hizi zitalipa ada ya kiingiio cha uanachama kiasi cha shilingi 50,000/= na ada ya mwisho wa mwezi kiasi ch shilingi 10,000/=.
e)      Kutakuwa na wanachama wa umoja ambao watakuwa ni Jumuiya, Taasisi, Klabu pamoja na Asasi zote za kiraia. Kiingilio ni shilingi 50,000/= na ada ya mwisho wa mwezi ni shilingi 10.000/=

2.      MASHARTI YA UANACHAMA
Ili mtu awe mwanachama wa MDI ni lazima akidhi vigezo vifuatavyo:
a)    Awe na umri kuanzia miaka 18, mwenye kupenda kujihusisha na shughuli za maendeleo;
b)    Awe na tabia njema na anayekubalika kwa jamii;
c)    Awe tayari kutumia muda wake na hata raslimali kwa shughuli za Jumuiya pale inapotakiwa;
d)    Awe tayari kulipa ada, kiingilio na michango mbalimbali kwa maendeleo ya Jumuiya.

3.      TARATIBU ZA KUOMBA UANACHAMA
a)      Kujaza fomu maalumu ya maombi ambayo itapatikana kwenye ofisi ya Katibu wa TWIKOMIGE. Majibu yatatolewa baada ya Mkutano Mkuu kujadili maombi ya mwanachama husika;
a)      Kulipa kiingilio cha uanachama kiasi cha shilingi Elfu Hamsini (Tshs50,000/=)
b)      Kuwa tayari kulipa ada ya shilingi Elfu Kumi kwa kila mwezi (Tshs10,000/=)

4.      HAKI ZA MWANACHAMA
Kila mwanachama ana haki ya:
a)      Kuchagua viongozi na kuomba kuchaguliwa katika uongozi;
b)      Kuwa huru kutoa maoni yake kuhusu uendeshaji wa shughuli za Jumuiya;
c)      Kujitetea kabla ya kuchukuliwa hatua na uongozi/wanachama;
d)     Kupata habarí/ taarifa za maendeleo na mwenendo wa shughuli zote zinazofanywa na Jumuiya kwa njia za uwazi.

5.      WAJIBU WA MWANACHAMA
Kila mwanachama ana wajibu wa:
a)      Kuhudhuria vikao vyote vya Jumuiya kwa mujibu wa Katiba hii;
b)      Kushiriki katika shughuli za Jumuiya kama itakavyoelekezwa na uongozi;
c)      Kutumia na kusimamia kwa uangalifu raslimali za Jumuiya;
d)     Kutoa kiingilio na michango mingine itakayopitishwa na vikao halali vya Jumuiya;
e)      Kutunza siri na taarifa nyeti za Jumuiya;
f)       Kutumia vizuri na kutunza rasilimali za Jumuiya.
.
6.      KUKOMA UANACHAMA
Uanachama utakoma kwa:
a)      Kutokana na kifo cha mwanachama;
b)      Kujiuzulu kwa hiari;
c)      Kutolipa ada kwa muda wa miezi sita mfululizo;
d)     Kutohudhuria vikao vitatu mfululizo bila taarifa kwa uongozi;
e)      Kufukuzwa kwa uamuzi wa wajumbe wa mkutano mkuu;
f)       Mwanchama yeyote, uanachama wake uliokoma kwa sababu zilizotajwa hapo juu hatarudishiwa kiingilio na michango yote aliyotoa;
g)      Mwanachama aliyefukuzwa akipenda kujiunga tena atalizimika kufuata masharti kama yalivyoainishwa katika kifungu hapo juu;
h)      Mwanchama aliyefukuzwa kwa makosa ya ugomvi, wizi au vitendo vyovyote; vinavyoweza kuaibisha, kuharibu na kutweza jina la Jumuiya, hataruhusiwa kujiunga tena na Jumuiya TWIKOMIGE.

7.     MLEZI KIUME/ KIKE
Kutakuwa na mlezi ambaye atatokana na wanachama wa heshima. Huyu atakuwa ni mshauri wa jumuiya yetu. Mlezi atapendekezwa na Mkutano Mkuu wa Jumuiya na jina lake kuhakikiwa na Mkutano Mkuu wa mwisho wa Mwaka.

8.      KUKOMA KWA ULEZI
Mwanachama atakoma kuwa mlezi kama kati ya mambo yafuatayo yatatokea:
a)    Kama atafariki;
b)    Kama kutakuwa na udanganyifu wowote katika uptishwaji wa Jina Lake;
c)    Matumizi mabaya ya madaraka;
d)    Kama atajiuzulu wadhifa huo baada ya kuandika barua kwa Katibu ya kuomba kufanya hivyo ndani ya siku 30;
e)    Matatizo ya kiafya;
f)     Baada ya kupatikana na hatia mahakamani na kufungwa jela kwa muda unaozidi miezi 6.



5.    IBARA 4
1.      MATAWI YA TWIKOMIGE
a)    Jumuiya inaweza kufungua matawi mbalimbali katika eneo laTanzania pale itakapoonekana kuwa ni sawa kutegemea na malengo ya umoja wetu;
b)   Tawi litafunguliwa pale tu ambapo mkutano mkuu utakuwa umeridhia kuanzishwa kwa tawi hilo na baadae kupitishwa na mkutano wa mwisho wa mwaka;
c)    Kila tawi litafanya shughuli zake kwa kutumia katiba hii lakini litaruhusiwa kuwa na kanuni zake mbalimbali ambazo hazitakuwa tofauti na malengo ya katiba hii;
d)   Mkutano mkuu utakuwa na uwezo wa kusimamisha shughuli za tawi lolote ambalo litakuwa linafanya shughuli zake kinyume na malengo ya katiba hii;
e)    Hakuna tawi lolote litakalokuwa nauwezo wa kubadilisha katiba hii au kuwa na katiba tofauti na katiba hii.

6.    IBARA 5
1.      VIONGOZI WA TWIKOMIGE
Kiongozi ni Mwanchama yeyote atakayepewa dhamana na wanachama kusimamia shughuli za Jumuiya, ama kwa kuchaguliwa au kuteuliwa na mamlaka husika.

2.     SIFA ZA KIONGOZI
a)    Awe mwanachama hai (wa jinsia yeyote) mwaminifu na mwadilifu;
b)    Awe anajua kusoma na kuandika na yupo tayari kujifunza na kujiendeleza;
c)    Mwenye uwezo wa kubuni na kusimamia shughuli binafsi na za jamii;
d)    Mwenye uwezo au kipaji cha kuwezesha watu kufanya kazi kwa ushirikiano.

3.     TARATIBU ZA UCHAGUZI WA UONGOZI
a)    Wanachama wenye nia ya kuwa viongozi wa Jumuiya watatuma maombi ya maandishi kwa nafasi za uongozi wanazotaka kushindania;.
b)    Viongozi watachaguliwa kwa kupigiwa kura za siri na wajumbe halali waliohudhuria katika Mkutano Mkuu;
c)    Uchaguzi utafanyika tu endapo idadi ya wajumbe wa halali kupiga kura ni nusu ya wanachama hai;
d)    Endapo wagombea wa nafasi ya uongozi watapata kura zinazolingana kwa mara ya kwanza, kura zitarudiwa kupigwa ili kupata mshindi;
e)    Endapo wagombea wa nafasi ya uongozi watafungana tena katika duru ya Pili ya uchaguzi, Mwenyekiti atatumia kura ya turufu kuamua ushindi.

4.     SAFU YA VIONGOZI
TWIKOMIGE itakuwa na safu ifuatayo ya uongozi:
a)      Mwenyekiti;
b)      Makamu mwenyekiti;
c)      Katibu;
d)     Katibu msaidizi;
e)      Mweka hazina;
f)       Mweka hazina msaidizi.
Viongozi wote watapatikana kwa njia ya kura ya siri wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwisho wa Mwaka.

5.     MUDA WA UONGOZI
a)      Muda wa viongozi kukaa madarakani ni miaka miwili mfululizo. Kiongozi anaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine;
b)      Katika kipindi cha tatu cha uongozi, theluthi moja ya viongozi wa zamani watalazimika kujiuzulu kutoa nafasi kwa wanachama wengine kushika nafasi za uongozi;
c)      Kiongozi anaweza kuachishwa uongozi endapo atakiuka masharti ya uongozi kulingana na kanuni zilizokubaliwa.

6.     WAJIBU WA VIONGOZI
i.            Mwenyekiti
a)    Atakuwa ndiye kiongozi mkuu wa umoja na ataongoza vikao vyote vya jumuiya na atakuwa na kura ya turufu;
b)    Atakuwa ndiye msemaji mkuu wa jumuiya;
c)    Atasimamia na kuhakikisha kuwa kazi zilizopangwa zinatekelezwa na wahusika na kwa muda muafaka;
d)    Atawakilisha au atateua mtu wa kuwakilisha Jumuiya katika mikutano na shughuli zingine nje ya Jumuiya;
e)    Atakuwa mwanzilishi wa ushirikiano na Jumuiya zingine;
f)     Atakuwa ni mjumbe wa bodi ya ushauri;
g)    Atakuwa mmoja wa waidhinishaji malipo na kuweka sahihi katika hati za malipo na hundi.

ii.            Makamu Mwenyekiti
a)    Atahudhuria vikao vyote vya jumuiya.
b)    Atafanya kazi zote zilizo tajwa katika sehemu ya 5.5.1 hapojuu endapo mwenyekiti hayupo.

iii.            Katibu
(a)    Ni mtendaji na mratibu wa shughuli za kila siku za Jumuiya;
(b)   Atakuwa mwandishi na mtunza kumbukumbu na nyaraka zote za Jumuiya;
(c)    Ataitisha mikutano yote ya Jumuiya kwa kushauriana na Mwenyekiti;
(d)   Atapokea maombi ya wanachama wapya na kuyawasilisha kwenye mkutano mkuu;
(e)    Atatoa taarifa ya shughuli za jumuiya katika mkutano mkuu wa wanachama wote;
(f)    Atakuwa mmoja wa waidhinishaji malipo na kuweka sahihi katika hati za malipo na hundi;
(g)   Atawajibika kwa Mwenyekiti wa Jumuiya.

iv.            Katibu msaidizi
Katibu msaidizi atafanya kazi kama ilivyoainishwa katika sehemuya (c) hapo juu anapotakiwa kufanya hivyo.

v.            Mweka Hazina
a)      Ni mtendaji na mratibu wa shughuli za kila siku za Jumuiya;
b)      Kupokea na kutunza fedha za Jumuiya na kutunza vitabu vya fedha;
c)      Kutayarisha taarifa za fedha (mapato na matumizi) na kuisoma katika mkutano wa wanachama wote;
d)     Atakuwa mmoja wa waidhinishaji na mweka sahihi katika hati za malipo na hundi;
e)      Ataratibu shughuli zote za kuongeza mtaji na kuinua uchumi wa Jumuiya na shughuli za wanachama;
f)       Mshauri mkuu wa vikundi vya wazalishaji na wajasiriamali.

vi.            Mweka Hazina msaidizi
Mweka Hazina msaidizi atafanya kazi kama ilivyoainishwa katikasehemu ya (e) hapo juu anapotakiwa kufanya hivyo.

7.    IBARA 6
1.     MIHIMILI YA JUMUIYA
Kutakuwa na kamati zifuatazo katika jumuiya:
a)     Kamati ya Utendaji;
b)    Mkutano Mkuu;
c)     Sekretariti
d)    Bodi ya Washauri.

                          i.            Kamati ya Utendaji
Kutakuwa na kamati ya utendaji itayoundwa na viongozi wote watano waandamizi wa TWIKOMIGE pamoja na wajumbe wengine 21 watakaochaguliwa wakati ule ule na kwa utaratibu ule ule wanavyopatikana viongozi waandamizi wa Jumuiya.

                       ii.            Kazi za Kamati ya Utendaji
a)      Ni chombo kitakachohusika kusimamia uendeshaji wa shughuli zote za kila siku za TWIKOMIGE;
b)      Ni muhimili utakaopanga kikao cha mkutano mkuu;
c)      Itakuwa na uwezo wa kutoa nguvu yake kwa kiongozi yeyote wa juu au kamati yeyote ndogo;
d)     Itakuwa na uwezo wa kusimamia na kuhakikisha kuwa utawala wa Jumuiya pamoja na fedha zake ziko katika mazingira yanayoheshimu Katiba;
e)      Itakuwa na uwezo wa kumusimamisha kiongozi yeyote wa juu wa Jumuiya au mshauri yeyote baada ya kupata ushahidi wa kutosha unaoonesha matumizi mabaya ya maadili ya madaraka, ufujaji wa fedha na mengine yanayofanana na hayo kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na kusubiri maamuzi ya mwisho ya mkutano mkuu;
f)       Kamati ya utendaji kwa madaraka yake au kwa ushauri wa wajumbe, inaweza kuunda nguvu kazi, kama itahitajika kwa ajili ya utendaji wa majukumu ya dharura kadri itakavyohitajika;
g)      Itakuwa ndicho chombo cha kutunga será za Jumuiya na itawajibika kwa utawala wa Jumuiya kwani itashiriki katika kutoa ushauri mbalimbali kwa viongozi ikiwa ni kisheria kwa wao kutekeleza majukumu yao.

                     iii.            Mkutano Mkuu
Kutakuwa na mkutano mkuu utakaojumuisha wajumbe wote wa kamati ya utendaji,
wawakilishi kutoka katika matawi yote ya Jumuiya, wanachama waasisi, wanachama wa heshima, wanachama wa umoja pamoja na marafiki mbalimbali waalikwa. Mkutano utafanyika tarehe 30 Mei kila mwaka.

                     iv.            Kazi za Mkutano Mkuu
a)      Ni muhimili unaochagua viongozi wa Jumuiya pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji;
b)      Utapitia bajeti ya mwaka ya Jumuiya na utapitisha bajeti ya mwaka unaofuata;
c)      Kujadili na kutoa mapendekezo kwenye ripoti ya Katibu mkuu;
d)     Utakuwa na uwezo wa kupitisha au kukataa majina yaliyopendekezwa kwa ajili ya walezi au washauri. Kufanya kazi zingine zozote kadri itakavyohitajika na Jumuiya;
e)      Itatoa miongozo na kanuni zote zinazo elekeza mahusiano na matawi mengine ya TWIKOMIGE na wanachama wote kwa ujumla.

                        v.            Sekretariati
Kamati ya utendaji itakuwa na mamlaka ya kuteua sekretariati kwa ajili ya kufanya kazi za kila siku za Jumuiya kadri itakavyohitajika. Sekretariati itaongozwa na viongozi wa Kamati ya utendaji ambao watasimamia shughuli zote za Sekretariati na itakuwa na mamlaka ya kutoa pesa kwa niaba ya Jumuiya nzima hadi kiwango ambacho kitaelekezwa na kamati ya utendaji.Sekretariati itawajibika kwa Katibu wa Jumuiya.

                     vi.            Bodi ya Washauri
Kutakuwa na Bodi ya washauri ya Jumuiya, ambayo itaundwa na wajumbe wawili hadi wanane kutoka nje au ndani ya Jumuiya. Wajumbe wa Bodi ya washauri watapendekezwa na kamati ya utendaji na watahakikiwa na mkuano wa mwisho wa mwaka. Wajumbe hao wa bodi ya ushauri watakuwa ni watu wenye tabia njema inayokubalika ndani ya Jumuiya, wawajibikaji na wako tayari kuindeleza wilaya ya Magu.

                   vii.            Kazi za Bodi ya Washauri
a)      Itawajibika kuhakikisha kuwa mali zote na mitaji ya Jumuiya ziko salama.
b)      Mali ya ya Jumuiya, aidha inayohamishika au isiyohamishika itakuwa mikononi mwa Bodi ya washauri na itakuwa na uwezo wa kushitaki au yenyewe kushitakiwa kwa sababu itakuwa na uwezo wa kukamilisha mikataba mbalimbali ya Jumuiya.
c)      Kwa mujibu wa Katiba hii, Bodi ya washauri itafanya kazi zake kwa kufuata Katiba hii pia na sheria zingine zinazohusiana na mambo ya ushauri Tanzania.

                viii.            Muda, Vipindi vya Bodi ya Washauri
a)      Wajumbe wa Bodi ya washauri watashika nafasi zao kwa muda wa miaka miwili (2) na wataruhusiwa kugombea tena kwa kipindi kingine cha pili;
b)      Bodi ya washauri itakutana mara mbili (2) kwa mwaka.;
c)      Bodi ya washauri watachagua M/Kiti wao kutokana na wajumbe wa Bodi ya wadhamini;
                      ix.            Kukoma kwa mjumbe kuwa Mshauri:
Mjumbe atakoma kuwa mshauri endapo mambo yafuatayo yatatokea:
a)      Kama atafariki;
b)      Kama atafanya kazi zake kinyume na utaratibu uliowekwa na Bodi;
c)      Kutumia vibaya madaraka yake;
d)     Kujiuzulu wadhifa wake kwa kutoa maelezo kwa maaandishi ndani ya siku thelethini (30) kwa kamati ya utendaji na kutoa nakala yake kwa wajumbe wa Bodi ya washauri;
e)      Akiwa na matatizo ya kiafya;
f)       Kupatikana na hatia mahakamani na kufungwa jela kwa muda usiopungua miezi sita (6);
g)      Bodi ya washauri itakuwa na nembo yake yenye maneno “Registrar Advisors of Magu Development Initiative (MDI)”;
h)      Washauri watalipa faida zote zitakazopatikana kutoka kwenye mali na miradi ya Jumuiya iliyowekezwa huko kwa Mhazini. Matumizi yoyote ya ziada katika mali hizo kwa uhakiki uliofanywa na Bodi ya washauri lazima itolewe taarifa yake kwa kamati ya utendaji ambayo itatoa ruhusa ya matumizi hayo ya fedha;
i)        Mshauri yeyote anaweza kutolewa katika nafasi yake na mkutano mkuu
wa mwisho wa mwaka kama shughuli zake zitaonekana kuingiza Jumuiya katika malumbano yasiyoisha. Nafasi zote zinazopatikana zitajazwa kwa utaratibu ule ule wa kawaida.

8.    IBARA 7
1.     VIKAO VYA JUMUIYA
Kutakuwa na vikao vya jumuiya kama ifuatavyo:
a)     Mkutano Mkuu;
b)    Mkutano wa Kamati ya Utendaji;
c)     Mkutano wa Dharura.


                          i.            Mkutano Mkuu wa mwisho wa Mwaka
(a)    Mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka utakuwa ndicho chombo pekee chenye nguvu ya juu katika Jumuiya kitakachowajibika kwa sera na kazi za Jumuiya kama ilivyoelezwa kwenye katiba hii;
(b)   Utakuwa na mamlaka ya kujibu hoja zote zilizowasilishwa kwake na mjumbe yeyote wa Jumuiya au kamati ya utendaji kwa kufuata utaratibu ulioainishwa katika Katiba hii;
(c)    Mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka utafanyika kati ya mwezi Desemba na mwisho mwa mwezi wa pili wa kila mwaka;
(d)   Kamati ya utendaji ndicho chombo kitakachowajibika kupanga agenda za mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka na kusambaza taarifa miongoni mwa wanachama mwezi mmoja kabla ya kikao ili kupata maoni pamoja na hoja nyingine mpya kama itakavyohitajika na wajumbe;
(e)    Taarifa kikao itasambazwa kwa wajumbe ndani ya siku 21 katika maandishi kwa wajumbee wote kuwataarifu kuhusu tarehe rasmi, muda, ukumbi na agenda ya kikao. Mambo yatakayojadiliwa kwenye kikao yatakuwa ni yale tu ambayo yako katika agenda na si vinginevyo na lazima yakubalike na wajumbe;
(f)    Mwenyekiti wa Jumuiya ndiye atakayeongoza mkutano mkuu waa mwisho wa mwaka.kama hatakuwepo, makamu Mwenyekiti atachukua nafasi yake.

Kama wote hawapo, basi mjumbe mwingine yeyote atachaguliwa kwa muda
ili kutekeleza majukumu hayo.



                       ii.            Mkutano wa kamati ya utendaji
(a)   Utakutana mara moja kila baada ya miezi miwili kama itakavyopangwa;
(b)   Utafanya kazi zake zingine kama ilivyopangwa kwenye katiba hiiI.



                     iii.            Mkutano wa Dharura
(a)    Mkutano mkuu wa dharura unaweza kuitishwa wakati wowote katika mwaka mbali na ule ambao umezoeleka mwishoni mwa mwaka;
(b)   Taarifa yake itatolewa siku 14 kabla kwa wajumbe wote wa mkutano mkuu;
(c)    Mapendekezo ya kuitisha mkutano wa dharura inabidi yaungwe mkono na angalau theluthi moja ya wajumbe wote wa mkutano mkuu na yapelekwe kwenye kamati ya utendaji ambayo ndiyo itaitisha mkutano huo;
(d)   Utashughulikia matatizo yote ambayo yatakuwa yanahitaji utekelezaji wa haraka wa mkutano mkuu.

9.    IBARA 8
1.     MWAJIRI WA JUMUIYA
Kamati ya utendaji ndiyo itakayoshika majukumu yote ya kuajili wafanyakazi au wataalamu wote wa Jumuiya. Pia wafanyakazi wale ambao wataifanyia kazi Jumuiya kwa muda fulani; pale ambapo hadidu rejea na masharti ya mwajiliwa yatasainiwa na pande zote. Waajiliwa wafuatao wataajiliwa na Jumuiya ya TWIKOMIGE:-
a)      Afisa wa programu/ Mkurugenzi;
b)      Afisa wa Utafiti;
c)      Watawala wasaidizi;
d)     Watumishi wa muda;
e)      Madreva.

10.                       IBARA 9
1.     FEDHA
                         i.            Vyanzo vya fedha
a)      Kiingilio na ada za wanachama;
b)      Michango kutoka kwa miradi ya wanachama inayodhamiwa na TWIKOMIGE;
c)      Misaada kutoka kwa wafadhili, serikali na wa tu binafsi;
d)     Mikopo na ruzuku zisizo na riba.

                       ii.            Usimamizi
a)      Jumuiya itafungua akaunti za fedha katika taasisi za fedha na benki;
b)      Fedha zote zinazokusanywa zitahifadhiwa benki kulingana na kanuni za fedha zilizopo
c)      Matumizi yote ya fedha lazima yaidhinishwe na mamlaka zilizokubalika katika kanuni za fedha na kutolewa stakabadhi husika;
d)     Taarifa za fedha zitatolewa kila baada ya miezi mitatu (3);
e)      Mwaka wa fedha utaanzia Januari 1 hadi Deseaba 31 ya mwaka husika;
f)       Mkutano mkuu utahakikisha kuwa vitabu vya fedha za jumuiya vimekaguliwa na wakaguzi wa ndani na nje wenye sifa zinazokubalika.

11.                       IBARA 10
1.     AKIDI
(a)    Akidi ya vikao vyote vya Jumuiya katika mihimili yote itakuwa ni mahudhurio ya walio wengi kutegemea na idadi ya wajumbe katika muhimili husika;
(b)   Kila mjumbe katika kila muhimili atakuwa na kura moja;
(c)    Katika vikao vyote vya Jumuiya Mwenyekiti ndiye kiongozi mkuu, asipokuwepo basi Makamu mwenyekiti atakaimu nafasi yake. Kama wote awapo, mjumbe yeyote atateuliwa kushika nafasi hiyo kwa muda;
(d)   Mwenyekiti kwa kutumia madaraka yake aliyopewa na katiba hii anaweza kusitisha michango zaidi kutoka upande wowote katika hoja yoyote iliyopo mezani;
(e)    Wakati wa uchaguzi kura zote zitakuwa za siri.




12.                       IBARA 11
1.     MAAMUZI
Maamuzi yote yatafanywa katika kikao kwa kufuata maamuzi ya wengi waliohudhuria katika kikao.

13.                        IBARA 12
1.      MAREKEBISHO YA KATIBA
a)      Katiba hii inaweza kufanyiwa marekebisho makubwa au kwa baadhi ya vipengele na mkutano mkuu;
b)      Mapendekezo ya azimio la kurekebisha katiba ni lazima yaungwe mkono na zaidi ya asilimia hamsini ya wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu;
c)      Marekebisho ya katiba yatawasilishwa kwa msajili wa Jumuiya za kiraia katika muda wa mwezi mmoja baada ya kupitishwa na wanachama.

14.                       IBARA 13
1.     NEMBO YA JUMUIYA
Nembo ya Jumuiya yetu itakuwa na maneno yafuatayo; “MAGU DEVELOPMENT INITIATIVE” (MDI) na itatumika katika makubaliano mbalimbali wakiwepo viongozi wawili na mshauri.

15.                       IBARA 14
1.     UKAGUZI WA AKAUNTI
Akaunti na makablasha yote yatakaguliwa wakati wanachama kumi (10) walioteuliwa rasmi kwa kazi hiyo wakishuhudia katika makao makuu ya Jumuiya na taarifa itatolewa ndani ya siku saba.


16.                       IBARA 15
      I.            KUVUNJIKA KWA JUMUIYA
a)      TWIKOMIGE inatarajiwa kufanya kazi zake kwa muda wote kulingana na mahitaji ya wanachama wake. Hata hivyo, TWIKOMIGE inaweza kuvunjwa endapo litapitishwa azimo la kuivunja ambalo litaungwa mkono na wajumbe halali wasiopungua theluthi mbili (2/3) ya waliohudhuria na kupiga kura katika Mkutano Mkuu;
b)      Kama akidi ya kuivunja TWIKOMIGE itakuwa haijafikiwa, pendekezo la kuivunja TWIKOMIGE litapelekwa katika mkutano mwingine utakaofuata;
c)      Akidi ya mkutano huu itakuwa ni 2/3 ya wajumbe;
d)     Hata hivyo pendekezo la kuivunja TWIKOMIGE litakamilika tu pale ambapo baada ya kupigiwa kura na wajumbe walio wengi litasainiwa na viongozi watatu waandamizi yaani Mwenyekiti, Katibu na Mhazini, na baadae kupelekwa kwa msajili wa vyama vya kiraia;
e)      Kama msajili atasaini pendekezo hilo, hakutakuwa na hatua zingine za ziada za kuchukua, isipokuwa ni kuivunja TWIKOMIGE moja kwa moja;
f)       Endapo TWIKOMIGE itavunjika, raslimali zake zitatolewa kwa Jumuiya nyingine inayofanya kazi zinazoendana na ndoto na malengo ya TWIKOMIGE;
g)      Bodi ya washauri, kwa kushirikiana na “Mfilisi” anayetambulika itahakiki mali za Jumuiya na kuwakilisha pendekezo la kukabidhi raslimali kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka.



No comments:

Post a Comment