Tuesday, March 19, 2013

Hatima ya dhamana ya Lwakatale Leo

MKURUGENZI wa Ulinzi na Usalama wa Chadema atapandishwa kizimbani leo kwa mara ya pili kwa ajili ya Hakimu kutoa uamuzi endapo atapata dhamana baada ya juzi dhamana yake kufungwa kutokana na kwamba anakabiliwa na kesi ya ugaidi.
Akisoma hati ya mashtaka juzi mbele ya Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru, Wakili wa Serikali Mkuu, Puldens Rweyongeza Wakili wa serikali alidai kuwa Lwakatale na mwenzake Ludovic Joseph , Desemba 28,2012 walishirikiana kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Msacky kinyume na kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi.
Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi kinyume na kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky.
Kwa mujibu wa shtaka la nne, Lwakatale anadaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kudai kuwa siku hiyo ya tukio, Lwakatale akiwa mwenye nyumba, akijua , aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick ufanyike katika nyumba yake kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya kigaidi dhidi ya Msacky. Baada ya kumaliza kusoma mashtaka hayo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu na wakili wa Serikali alidai kuwa kesi hiyo haina dhamana.
Pia aliiomba mahakama kuruhusu mshtakiwa Ludovick kupelekwa polisi kuendelea na shughuli za upelelezi.Lwakatale anatetewa na mawakili, Peter Kibatara, Mabere Marando, Abdallah Safari, Nyaronyo Kichere na Tundu Lisu.

Lwakatale mbele (kushoto) na Ludovic mwenye shati nyeusi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Askari Polisi jana kisutu
Wakili wa utetezi Kibatara aliiomba mahakama kutoa dhamana kwa mteja wao kulingana na mazingira husika na kwamba izingatie kuwa dhamana ni haki ya msingi ya washtakiwa. Kibatara alidai kuwa ugaidi siyo kosa dogo ni kitu kikubwa iwapo chombo cha kisheria kinachukua haki ya mtu ya dhamana ni lazima kuwepo na sababu zinazojitosheleza kuwa mtu huyu kweli ni hatari na mahakama iridhie kweli ni hatari anyimwe dhamana.

Wafuasi wa Chadema wakionyesha ishara ya vidole viwili katika chumba cha Mahakama ya Hakimu mkazi kisutu jana jijini Dar es Salaam
Wakili Lisu aliunga mkono hoja za wakili Kibatara. Kwa upande wa wakili Abdallah Safari aliitaka mahakama ichukue kumbukumbu kuwa vitendo vya kubambikia kesi watu vimekithiri katika nchi hii. Hakimu Mchauro atatoa uamuzi juu ya hoja hizo Jumatano ya Machi 20 leo, mwaka huu kama washtakiwa hao watapata dhamana ama la.

No comments:

Post a Comment