Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
(Tas) mkoani Mwanza, kimelaani vikali kitendo cha familia moja wilayani
Magu kumzika ndani ya chumba cha biashara mtoto wao mwenye ulemavu wa
ngozi (albino).
Mtoto huyo aliaga dunia Desemba 15, mwaka jana nyumbani kwao mjini Magu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Mwenyekiti wa Tas
Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, alisema kimsingi chama chake
hakikubaliani na kitendo hicho ambacho kilifanyika usiku wa manane bila
kuishirikisha jamii ya eneo husika.
Kapole, ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wenzake wa chama hicho
mkoani Mwanza na taifa, alisema hatua yao ya kulaani kitendo hicho
inatokana na ukweli kuwa inaweza kuchochea mauaji dhidi ya albino.
Alifafanua kuwa wiki iliyopita, alipokea taarifa kutoka wilayani Magu
kuwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Witness Edward Omari, mwenye umri wa
miaka miwili na miezi saba, mkazi wa mtaa wa Isandula mjini Magu,
amefariki dunia na mwili wake kuzikwa ndani ya chumba cha biashara
kinachomilikiwa na baba yake.
Aidha, alisema taarifa hizo zilieleza kuwa siyo tu kwamba mtoto huyo
alizikwa ndani ya chumba cha duka, bali pia kitendo hicho kilifanywa
usiku wa manane bila jamii ya eneo husika kushirikishwa.
“Nilipigiwa simu na mwenzetu mmoja kutoka Magu akaniambia kwamba baada
ya Witness kufariki dunia, alizikwa ndani ya chumba cha duka, na kweli
tulipokwenda kuitembelea familia yake, tuliingizwa ndani ya chumba hicho
kuonyeshwa kaburi lake,”alisema Kapole.
Aliongeza kwamba taarifa zaidi walizozipata zinasema kuwa mwili wa mtoto
huyo ulichukuliwa na wazazi wake kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha
Hospitali ya Wilaya ya Magu Desemba 16, mwaka jana majira ya usiku kwa
ajili ya kwenda kuuzika.
Ofisa Uhusiano wa Tas taifa, Josephat Toner, alisema wao kama jamii ya
albino, hawakubaliani na kitendo hicho kwa sababu kinakiuka misingi ya
ubinadamu na pia kinaweza kuchochea mauaji dhidi yao.
Alisema katika jamii nyingi za Watanzania, wanaamini kuwa albino hawafi
kifo cha kawaida bali hupotea, hali ambayo imekuwa ikichochea mauaji
dhidi yao kwa baadhi ya watu kudhani kuwa viungo vyao si vya kawaida na
vinaweza kusababisha utajiri.
Kwa msingi huo, alisema kitendo cha familia ya Witness kumzika mtoto wao
ndani ya chumba cha biashara tena usiku wa manane pasipo kuishirikisha
jamii, kinaweza kuchochea imani hiyo potofu kwamba albino hawafi bali
hupotea.
“Albino ni binadamu kama binadamu wengine, tunazaliwa na kufa, hivyo
mazishi yetu yanapaswa kufanyika hadharani kama vile mazishi ya watu
wengine yanavyofanyika, lazima `wananzengo' (wanajamii) washiriki kwa
taratibu zilizozoeleka ili kuondoa kabisa dhana potofu kwamba hatufi
bali tunapotea,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Tas Mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju, alisema
kitendo kilichofanywa na familia ya Witness, kimewatia simanzi kiasi cha
kuwafanya wawe na hisia mbaya dhidi ya familia hiyo.
Alifafanua kwamba ingawa Witness alikufa kifo cha kawaida baada ya
kuugua kwa muda mfupi, lakini namna ambavyo mwili wake umezikwa ndiko
kunakowatia shaka na kuhisi kuwa huenda kuna jambo limejificha.
Alisema kama lengo la familia hiyo lilikuwa kuepusha uwezekano wa watu
wenye imani potofu kufukua kaburi la mtoto wao, ni bora wangemzika
katika makaburi ya jamii na kujengea zege lakini sio kumzika ndani ya
chumba cha biashara tena kwa siri.
“Kutokana na mazingira ya tukio lenyewe, kama chama tumeamua kufungua
jalada la shaka na kuiomba mahakama itoe kibali kwa Jeshi la Polisi
kufukua kaburi la Witness ili tujiridhishe iwapo kweli mwili wake una
viungo kamili kwa sababu hata mahali penyewe tulipoonyeshwa kuwa ndipo
alipozikwa, hapaonyeshi dalili hizo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema hajapata taarifa.
Hata hivyo, alisema kama tukio hilo lipo ni vema viongozi wa Tas wakamuona Mkuu wa Polisi Wilaya ya Magu ili alishughulikie.
“Mimi sina taarifa pengine Tas walikuja ofisini wakati nimetoka, lakini
nitafuatilia kujua kama walizungumza na wasaidizi wangu ili tumwelekeze
OCD alishughulikie ingawa suala la kufukua kaburi linahitaji kwanza
kibali cha mahakama,” alisema Kamanda Mangu.
No comments:
Post a Comment