Thursday, January 24, 2013

Wanafunzi, walimu kujisadia vichakani ni aibu ya taifa

 CHANZO NIPASHE
Katika toleo la jana 24/01/2013 la gazeti hili ukurasa wa 16 kulikuwa na habari ya kuchefua, kukasirisha na kukatisha tamaa, kwamba wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Nampemba iliyopo Kata ya Nambambo Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wako hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko kutokana na kujisaidia vichakani kwa kukosa vyoo.

Habari hiyo ilisema kuwa shule hiyo ya kijiji cha Nampemba iliyojengwa kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) haina vyoo kwa kipindi cha miaka saba, hali hiyo inawaacha wanafunzi na walimu wao kujisitiri vichakani. Yaani ndani ya miaka 51 ya Uhuru bado hatuwezi kujenga choo!

Hakuna binadamu yeyote mstaarabu ambaye hajui maana ya kuwa na choo na kukitumia. Hakuna. Hali inakuwa ni ya kushangaza na kuchefua zaidi kundi linalokuwa halina choo kuwa ni la wanafunzi na walimu, yaani shule ambayo inapaswa kuwa kitovu cha ustaarabu na kuelemisha jamii juu ya madhara ya kutokuwa na choo, ndiyo inakosa huduma hiyo muhimu kwa afya ya binadamu.

Ni hakika kama walimu na wanafunzi hawa hawajaanza kuugua magonjwa ya milipuko kama kuhara, kipindupindu na mengine ya tumbo, basi wana bahati ya mtende kwa kuwa kujisaidia ovyo vichakani ni sawa kabisa na kuendelea kuukaribisha uchafu huo kwenye vyakula na maji wanayotumia.

Katika eneo lote la nchi hii hakuna hata kipande cha sentimeta moja ambacho hakina kiongozi.

Kila ukikaribia wakati wa uchaguzi watu wanapigana vikumbo kusaka uongozi wa kuchaguliwa, hawa ni kuanzia wajumbe wa kamati za utawala ngazi ya vijiji na mitaa, wenyeviti wao na kuna watendaji wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi. Hawa ni watendaji wa vijiji, mitaa na kata. Hawa ndiwo wasimamizi wakuu wa shughuli za maendeleo katika maeneo yao. Wapo wamejaa lakini hawafanyi lolote!

Mbali na viongozi hao, shule hii ina walimu, yupo mwalimu mkuu, wapo wanafunzi ambao wana wazazi. Wote hawa kwa ujumla wao kwa miaka saba wameshindwa kujenga choo cha shimo katika shule hii ili wanaotoa huduma na kuhudumiwa na shule hii waishi maisha ya staha kwa kuwa na mahali pa kujisitiri.

Mara nyingi tumejiuliza maswali ambayo majibu yake hayapatikani kwamba hivi hawa wanaokimbilia kusaka madaraka ya uongozi katika nchi hii kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi juu baadhi yao wanakuwa wanawaza nini? Ni kutumika au kutumikiwa?

Inashangaza kuona kwamba eti
mwenyekiti wa kijiji hicho bila aibu anakwepa wajibu wa kazi hii kwa kuitupia lawama Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa madai kuwa ndiyo chanzo cha ukosefu wa choo katika shule hiyo.

Kwamba kijiji kizima kwa miaka saba kimeshindwa kujenga choo cha shule, ni utetezi unaoacha maswali magumu ya uwajibikaji kwa watu wanaosaka madaraka ya umma, lakini wakishakalia viti hivyo hawana wanalofanya mbali ya kuendekeza ubinafsi.

Kadhalika, kama kijiji kinaweza kuruhusu shule iendeshwe bila choo, inatupa hofu kwamba hata wanavijiji kwa ujumla wao suala la vyoo siyo la kipaumbele katika maisha yao; tunajiuliza kama makazi yao yana vyoo vya kueleweka. Hofu hii inapata mashiko kwa sababu kama wangelikuwa wanajua umuhimu wa vyoo kiasi hicho, basi wasingelikubali kuona shule wanayosama watoto wao ikiachwa katika ukiwa kama huo.

Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea hakina tunakosa maneno ya kusema, kwamba miaka saba imeshindwa kuisaidia shule ya msingi kuwa na choo? Katika nchi zinazojali uwajibikaji baraza zima la madiwani na mkurugenzi wa halmashauri walipaswa kuachia hazi kwa uzembe huu ambao unakera na kutia kichefuchefu.

Tunajiuliza maswali mengi kama kweli hatuwezi kujenga choo na kukitumia kwenye shule zetu, hivi tunaweza kutoa elimu ya namna gani basi? Tunakua na ujasiri gani wa kuamini kwamba tunaweza kushindana katika dunia hii inayosukwasukwa na changamoto za utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya kompyuta?

Itoshe tu kusema kuwa Halmashauri ya Nachingwea, wanakijiji na uongozi mzima cha Nampemba na uongozi shule ya msingi hiyo hakika wanaidhalilisha Tanzania kwa kuishi bila choo. Hali hii kwa ukweli haikubaliki na ni moja ya kipimo cha chini kabisa wote wanaojiita viongozi kwenye mnyororo wa madaraka kuanzia halmashauri, kijijini na shuleni kuwa wameshindwa kazi.

Kama kiongozi hawezi kusimamia ujenzi na matumizi ya choo kwenye eneo lake la utawala hivi anaweza kufanya nini basi kama kiongozi?

CHANZO NIPASHE.

No comments:

Post a Comment