RAIS wa Shirikisho la Wakulima wa Afrika Mashariki, Philip Kiriro, amewataka
wakulima wadogo kuungana katika kupigania maslahi yao, ili kujikomboa kutoka
kwenye ukulima mdogo hadi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kiriro alisema
iwapo wakulima hao hawataungana mafanikio yao hayatakuwa mbali.
Alisema shirikisho hilo lenye makao makuu nchini Kenya, limekusudia
kuwaunganisha wakulima kwa lengo la kuwa na sauti moja katika maamuzi yao
ambapo litafanya kazi na serikari za nchi hizo.
“Tumekuja hapa nchini kukutana na Shirikisho la Vyama Ushirika, pia
kutembelea ofisi za serikali na kuifahamisha serikali juu ya shirikisho hilo
litakavyofanya kazi na wakulima wadogo katika nchi za Afrika Mashariki,”
alisema Kiriro.
Aidha alisema kati ya nchi zilizopo kwenye jumuia hiyo, Tanzania ina fursa
ya kufanya vizuri katika kilimo kutokana na kuwa na maeneo makubwa kwa shughuli
za kilimo.
Naye Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TCC), Willings
Mbogo, alisema watahakikisha kupitia shirikisho hilo wanakuza uwezo wa wakulima
wadogo na wajasiriamali, ili waweze kukuza uchumi kutoka katika hali ya sasa na
kuufanya uwe bora zaidi.
No comments:
Post a Comment