TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepongezwa kwa jitihada
inazochukua hivi sasa kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakuwa imara, sauti moja na
hivyo kuchangia zaidi katika ujenzi wa uchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Mwanza hivi karibuni, Jovita Bubere
na Moses Nyaronga, walisema TPSF imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara
zao na kuongeza mitaji.
“Tunaomba taasisi hii iendelee na jitihada zake za kuwasaidia wanachama wake
mikoani, ili kuendelea kutujenga katika kukuza biashara hasa kwa mikutano kama
hii ya kikanda,” alisema Bubere wakati wa mkutano ulioshirikisha wanachama wa
TPSF Kanda ya Ziwa.
Bubere ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya kinamama Wajasiriamali Tanzania,
alisema: “Tunahitaji msaada mkubwa ili kuweza kufikia malengo yetu.”
Akizungumzia soko la Afrika Mashariki, mwenyekiti huyo alisema wamejipanga
vizuri na tayari wameshaanza kutoa mafunzo kwa baadhi ya kinamama kuhusiana na
mbinu za kutumia ushindani unaokuja wa kibiashara.
Kwa upande wake, Nyaronga ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la Lemon
Development Foundation lililoko katika wilaya ya Rolya, mkoani Mara, alisema
huu ndio wakati wa kuiunga mkono TPSF, ili iweze kufanya kazi kwa uhakika zaidi
ya ilivyo sasa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Geofrey Simbeye, alisema taasisi hiyo
ina lengo la kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wanachama wake katika kuongeza
kasi ya uanzishwaji wa makampuni na viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira na
kuinua uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment