Wednesday, March 20, 2013

Wasimamizi afya ya uzazi wapatiwa kompyuta

SHIRIKA lisilo la kiserikali Tandabui Health Access Tanzania (THAT)/Afya radio la jijini Mwanza limekabidhi kompyuta nne zenye thamani ya sh milioni 4.4 kwa wasimamizi wa huduma ya afya ya uzazi mkoa wa Mwanza na wilaya ya Ilemela, Geita na Nyamagana, ili kuboresha huduma hiyo.
Akikabidhi kompyuta hizo kwa mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, waganga wakuu wa wilaya za Ilemela, Nyamagana na mratibu wa afya ya uzazi wilaya ya Geita, meneja miradi wa shirika hilo, Doto Biteko, alisema lengo la kutoa kompyuta hizo ni kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na wasimamizi hao katika kufikia upatikanaji wa huduma bora.
Alisema kompyuta hizo zimeunganishwa na mfumo wa mawasiliano wa shirika hilo unaoratibu ubora wa huduma zitolewazo kwa wajawazito kwenye vituo vya afya, ili kuwawezesha wasimamizi na waratibu hao kupata taarifa za moja kwa moja kutoka kwa wananchi.
Aliongeza kuwa mfumo huo unakusudia kuongeza kasi ya uwajibikaji wa wasimamizi wa huduma za afya hasa za mama na mtoto kutokana na taarifa za utolewaji wa huduma vituoni kuwafikia kwa muda muafaka na bila kuhaririwa.

No comments:

Post a Comment