Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela akifafanua jambo |
Wakati Waziri Mkuu Mstaafu, John
Malecela ameonya Watanzania kuhusu mpasuko wa kidini akibainisha kuwa utaigawa
nchi vipande vipande, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ametoa wito maalumu
akiwataka waumini wa dini tofauti kuvumiliana.
Malecela na Mwinyi walitoa kauli
hizo mjini Dodoma na Kibaha, Pwani jana kwa nyakati tofauti, wote wakiwa na nia
ya kusisitiza ulinzi wa amani ya nchi inayoanza kutetereka.
Kauli ya Malecela
Malecela alisema kwa namna ilivyo
sasa, Tanzania imekuwa ni tofauti na ile aliyoanza kuiona yeye katika kipindi
cha uhuru kwenye miaka ya 1960 wakati huo nchi ikiwa moja na watu wake wakiwa
ni wamoja.
“Msipokuwa makini na amani yenu,
nchi hii mtaigawa vipande vipande na kamwe amani ya kweli haiwezi kupatikana
kwa mambo ya kusingiziana, badala yake tusaidiane sisi kwa sisi, na sisi na
viongozi,” alisema.
Onyo la Malecela limekuja kutokana
na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mpasuko wa kidini unaoanza
kujitokeza nchini.
Malecela alieleza wasiwasi wake juu
ya tofauti za kidini katika ibada maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika
Kanisa Anglikana Chiwondo lililoko kijiji cha Hombolo katika Manispaa ya
Dodoma.
Anafuata nyayo za viongozi wa
kitaifa walioonya masuala ya udini kama Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Marais wastaafu, Mwinyi na Benjamin
Mkapa pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Alisema waliovamia na kupiga bomu
kanisani Arusha ambapo Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla
alinusurika kuuawa, si wajinga na wanaweza kufanya mambo kama hayo eneo lolote
nchini.
“Kujenga nchi ni kazi ngumu
sana lakini kuibomoa ni kitendo cha muda mfupi ambacho kinaweza kufanyika kwa
kutumia sekunde chache ni lazima kuisaidia serikali katika kuitafuta amani,”
aliongeza Malecela.
Malecela ameonya baadhi ya
watu kutochukua sheria mikononi kuhusu yale yanayowapata na badala yake
waiachie Serikali yao kufanya uamuzi wa nini kifanyike ili amani ibaki.
Kwa upande wake Rais Mstaafu Mwinyi alisisitiza amani idumishwe na kuwataka Waislamu na Wakristo kupendana na kuvumiliana ili jamii iweze kuishi bila hofu.
“Haiwezekani dini moja kuitaka dini nyingine isiwepo,” alisisitiza Mwinyi. Mwinyi alitoa msisitizo huo jana mjini Kibaha wakati akitoa mawaidha yaliyolenga kusisitiza amani nchini kufuatia matukio kadhaa yaliyoripotiwa kutokea nchini na kudaiwa yanahusiana na masuala ya kidini.
Alisema si ajabu kukuta hata sasa baadhi ya watu wameingiwa na hofu na waumini wakisikia kitu hata kama ni paka wanakimbia na kuacha mahubiri.
“Hakuna sababu ya kutufikisha hapo jamani, mbona dini hazijaanza leo? Tangu enzi watu wanaabudu kila mtu kwa imani yake, watu wanaoana, wanakula pamoja, wapo ofisi moja, magari wanapanda pamoja sasa iweje hii itokee leo hii?” alihoji Mwinyi.
No comments:
Post a Comment